Home / Habari Za Kitaifa / Serikali kuwatumia waliogombea EALA

Serikali kuwatumia waliogombea EALA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema itaendelea kuwatumia wananchi walioshiriki katika mchakato wa kuwania nafasi mbili za kuiwakilisha Zanzibar katika Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EALA) kutokana na upeo wa maarifa waliyonayo yaliyodhihirisha kulitumikia taifa kizalendo.

Wanachama 34 wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wenye ujuzi na sifa tofauti waligombea EALA na kupatikana wenzao wawili Maryam Ussi Yahya pamoja na Abdallah Hasnuu Makame kupeperusha bendera ya Zanzibar katika bunge hilo.

Akizungumza na wanachama hao, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza na kusema taifa linatambua uwezo na sifa walizonazo wanachama hao kiasi kwamba serikali itaendelea kuwatumia.

Alisema upo umuhimu kwa wasomi hao wa CCM kuendelea kukitumikia chama chao katika mfumo wa kitaaluma zaidi kutokana na uwezo wa chama hicho katika ukombozi wa Bara la Afrika na dunia kwa ujumla.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa pongezi za dhati kwa kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo ambayo imedhihirisha kwamba kumbe wapo viongozi wengine zaidi wenye sifa na uwezo mkubwa,” alisema.

Aidha aliwataka wabunge wastaafu kutumia muda wa kupumzika kwa ajili ya kutoa michango mbalimbali ili taifa liweze kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar.

Akitoa shukrani zake kwa CCM, Mbunge mteule wa Afrika ya Mashariki, Maryam Ussi Yahya alisema wamejipanga vizuri kutetea maslahi ya Zanzibar katika Bunge la Afrika ya Mashariki na kuona miradi iliyopewa kipaumbele inatekelezwa vizuri.

Alisema akiwa Mbunge kwa kipindi cha pili katika Bunge hilo, alisema Zanzibar inayo fursa kubwa na kufaidika na miradi ya jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na biashara.

Aidha Mbunge mteule mpya, Makame alisema atatumia uzoefu wake wa kufanya kazi katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuona Zanzibar inafaidika na fursa zilizomo katika jumuiya hiyo kiuchumi na maendeleo.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *