Home / Habari Za Kitaifa / Familia yatengwa kwa ugonjwa wa ngozi

Familia yatengwa kwa ugonjwa wa ngozi

WAKAZI wa kitongoji cha Nkata kilichopo katika kijiji cha Kate, Kata ya Kate katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wameingiwa na hofu kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa ngozi, uliowakumba watu wanane wa familia moja kijijini humo.

Gazeti hili lilibaini hayo baada ya kufanya mazungumzo na Paroko wa Kanisa Katoliki, lililopo katika kata ya Kate, Padre Jofrey Kitaya ambaye alimwokota mtoto Peter Kazumba (13), aliyelala usiku kucha pembezoni mwa Zahanati ya Mtakatifu Anna, inayomilikiwa na Watawa wa Kanisa Katoliki iliyopo katika kijiji cha Kate .

Mtoto Peter ambaye hasomi na hajawahi kuingia darasani, anasumbuliwa na ugonjwa sugu wa ngozi, ambao umemfanya aharibike na kutoa harufu kali, huku akiwa na jeraha kubwa la moto katika goti lake la mguu wa kushoto na anaonekana mzee kuliko umri wake.

Gazeti hili lilifunga safari umbali wa kilometa 60 kutoka Sumbawanga mjini hadi Parokia hiyo ya Kate na kukutana na Padri Kitaya, kisha kufunga safari zaidi ya kilomita nne hadi katika kitongoji cha Nkata, nyumbani inakoishi familia ya mtoto huyo.

“Ilikuwa Jumatatu ya Pasaka asubuhi nilikuwa nimetoka kuongoza ibada ya Misa Takatifu, basi nikashuka hadi zahanati ndipo nilipomwona mtoto huyu akiwa amelala pembeni mwa ukuta wa zahanati.

Jinsi alivyoharibika mwili wake, nilidhani ama nimetokewa na Yesu Mfufuka katika sura ya mateso au Lazaro, sikuamini macho yangu nilipatwa na mshtuko mkubwa mno, kwani inahitaji imani ya ziada kuzungumza na mtoto huyo jinsi alivyo .

Nilimchukua hadi kwa watawa wa Kanisa Katoliki hapa Kate, wakampatia kinywaji baridi na keki kwa jinsi alivyokuwa anakula ni wazi alikuwa amebanwa na njaa na kiu,” alisema Padri Kitaya.

Gazeti hili lilifika kijijini Kate juzi Jumanne na Padri Kitaya alifuatana na gazeti hili hadi katika zahanati ya Mtakatifu Anna, kwa matumaini yan kukutana na mtoto Peter. Lakini, baadhi ya wagonjwa waliokuwa hospitalini hapo, walieleza kuwa amechukuliwa na baba yake mzazi.

Kutokana na taarifa hiyo, gazeti hili, Padri na mganga wa Kituo cha Afya cha Kate, Peter Abdalah, walielekea katika kitongoji cha Nkata na kukutana na mtoto huyo, baba mzazi na majirani ambao katika mazungumzo yao, walihusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Martin Kazumba (36) alidai kuwa amekuwa akimpeleka mtoto wake huyo katika Kituo cha Afya kilichopo katika kijiji jirani cha Mvimwa wilayani Nkasi, kwa matibabu kwa miaka mitano mfululizo bila mafanikio.

“Tayari nimefilisika kwa ajili ya kugharamia matibabu ya mtoto wangu huyu, amekuwa akitibiwa kwa miaka mitano mfululizo bila kupona huku hali yake ikiendelea kuwa mbaya kila kukicha.

Isitoshe mke wangu, mimi mwenyewe na watoto wengine watano, akiwemo wa mwaka, tumeshaambukizwa ugonjwa huu. Nimekata tamaa sijui la kufanya hakika nimechoka inawezekana tumerogwa kwa nini ni sisi tu yaani hii familia yangu pekee ?” alihoji.

Wakati hayo yakijiri mama mzazi wa mtoto Peter pamoja na watoto wengine, walikuwa shambani mbali na kijiji hicho. Kwa upande wake, mtoto Peter alimwomba Rais John Magufuli na wasamaria wema, waguswe na ugonjwa alionao, ambao unampatia mateso makubwa, wamsaidie gharama za matibabu.

Akizungumza kwa taabu, alisema, “Sina raha kabisa kuendelea kuishi kwa kuwa hata majirani zetu wananitenga, watoto wenzangu pia hawako tayari kucheza wala kula na mimi”. Baadhi ya wakazi waliozungumza na gazeti hili kijijini hapo kwa nyakati tofauti, walikiri kuingiwa na hofu kubwa ya kuweza kuambukizwa ugonjwa huo, waliouita wa ajabu.

“Sio siri tunaogopa hata kwenda kumjulia hali jirani yetu tukihofia kuambukizwa ugonjwa huo. Kijiji kinaamini hauna tiba,” alieleza mkazi wa kijiji hicho, Ignas Kipeta. Akizungumza, Padri Kitaya alisema, “ Wapendwa Taifa la Mungu, sote tuguswe na madhira yaliyompata mtoto huyu (Peter) na familia yake , si kazi rahisi kwa mtu mmoja pekee bali Serikali, kanisa, taasisi mbalimbali na watu binafsi, tuguswe na kujitokeza kuisaidia familia hii ambayo imekubikwa na mateso makubwa ya kimwili na kiroho”.

Kwa upande wake, Mganga wa Kituo cha Afya cha Kate, Abdallah alieleza kuwa ugonjwa huo kitatibu unajulikana kama Adematomycosis na kwamba mtoto huyo amepatwa na usugu wa ugonjwa huo wa ngozi, unaosababishwa na fangasi.

“Ugonjwa huu ni hatari kwa sababu unaambukiza na unaweza kuenea kirahisi katika jamii nzima na kusambaa zaidi lakini licha ya kuwa ni hatari bado unatibika. Tatizo mtoto huyu hawezi kulazwa kwa matibabu katika zahanati na vituo vya afya kwani anahitaji uangalizi maalumu. Nashauri apelekwe katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa iliyoko katika Mji wa Sumbawanga, ambako kuna wataalamu, mtoto huyu anatakiwa awe chini ya uangalizi wa jopo la wataalamu wa afya,” alisema.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *