Home / Habari Za Kitaifa / Lusinde awataka wabunge kuheshimiana

Lusinde awataka wabunge kuheshimiana

MBUNGE wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde amewataka wabunge kujiheshimu na kuheshimu wenzao, kama kweli wanataka kuheshimika huku akilaani kitendo cha mbunge wa chama hicho, Dk Godwin Mollel kupuuza hatua zinazochukuliwa dhidi ya watu wanaochukuliwa hatua kwa kumtukana Rais John Magufuli kupitia mitandao.

Alisema inashangaza kuona mbunge huyo akitaka Serikali iache kushughulika na mambo yanayoitwa madogo, yakiwemo kama ya kumtukana Rais. Awali, akichangia hotuba za bajeti za wizara mbili zilizopo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na ile ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Mollel ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Siha, aliwataka Watanzania kubadilisha fikra, huku upande serikalii akiisihi iache kushughulika na mambo madogo, akitolea mfano wanaoshughulikiwa kwa kumtusi Rais.

Lakini Lusinde, alikemea hilo, akisema; “Haiwezekani Rais atukanwe, halafu Mbowe aheshimiwe…Rais anafanya kazi kubwa sana ya kubadilisha mfumo wa uongozi wa nchi hii… Dokta (Mollel) hapa amezungumzia suala la kubadilisha fikra, na huu ni mchango wake wa pili wa aina hii, anasisitiza hilo, kwanza tuwe na mtazamo mpya ili tusonge mbele….

“Anasema tuache kushughulika na watu wadogo wanaomtukana Rais na badala yake tuhangaike na mambo makubwa…aah, ila dokta huyo huyo anayetutaka tubadilishe fikra anasema kiongozi wa kambi ya upinzani aheshimiwe, ni mtu mkubwa. Yaani Rais atukanwe, Mbowe aheshimiwe? Hatuwezi kwenda hivyo, kama tunataka heshima. Tukiheshimiana hapo tutaona kuendesha nchi ni kazi rahisi.”

Alisisitiza suala la kutukanwa si dogo, hivyo viongozi wa vyama vingine vya upinzan wasilee matukio ya aina hiyo, bali waungane kumuunga mkono Rais na serikali yake kwa ajili ya ustawi wa nchi. “Mimi naamini Rais anafanya kazi nzuri kabisa ya kuubadilisha mfumo wa nchi hii. Kazi yetu kubwa isiwe kumrudisha nyuma, tumpe moyo, tumtie nguvu Rais wetu, tuwatie nguvu mawaziri wasukume mbele gurudumu la maendeleo.

“Hivyo naomba tunapozungumzia heshima tuzungumzie pande zote mbili,” alisema na kuimwagia sifa serikali kuwa inafanya kazi kubwa kiutendaji, akitolea mfano Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Kazi inavyozikabili kero za ardhi. Akikazia suala la heshima, alisema anasikia kuna mbunge wa upinzani (Joshua Nassari wa Chadema) juzi aliingia maeneo ya Bunge akiwa na pombe aina ya Konyagi, hivyo kutaka awajibishwe na chama chake.

“Sisi juzi juzi tu hapa Serikali imemwajibisha Kitwanga (Charles, aliyevuliwa Uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) kwa kudhaniwa tu amelewa, lakini leo mbunge anaingia na konyagi maeneo ya bunge na anakamatwa. “Sasa leo hii tunataka kuona meno yenu yako wapi, kwa kumwajibisha huyo mbunge, kama mtaweza maana kazi yenu ni kusema tu siyo kutenda. Tunataka kuona mtakuwa wakali kwa kiwango gani kwa mbunge anayekuja bungeni amelewa halafu ana chupa ya konyagi. Sisi tumeshaonesha njia, waziri amekuja amelewa amewajibishwa, sasa ninyi mtachukua hatua gani? alihoji.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *