Home / Habari Za Kitaifa / Sababu Shein kupongeza Polisi Z’bar

Sababu Shein kupongeza Polisi Z’bar

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amelipongeza Jeshi la Polisi Tanzania kwa kuendelea kusimamia vyema amani na utulivu Zanzibar.

Akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi, Shein alisema Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi kubwa katika kuhakikisha amani na utulivu inaimarishwa na wananchi wanajishughulisha na shughuli zao za kijamii wakiwa salama.

Alisema Jeshi hilo Visiwani Zanzibar limekuwa likitekeleza vema kazi zake na kutoa ushirikiano mzuri kwa wananchi huku akisisitiza kuwa, ipo haja kuongeza ari hiyo ili lizidi kuitumikia vema jamii.

Rais Shein alisema ana matumaini makubwa kwa uongozi wa IGP Sirro na kumuahidi kuwa ataendelea kushirikiana naye pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili Jeshi hilo lizidi kupata maendeleo sambamba na kusimamia vema amani na utulivu.

“Nataka nikuhakikishie kuwa mimi na Rais John Magufuli tuna imani na matumaini makubwa na uongozi wako hasa tukitambua ari yako ya utendaji wa kazi, hivyo tuna imani kuwa Jeshi la Polisi litazidi kuimarika na mimi nakuahidi nitaendelea kukupa mashirikiano yote,” alisema Shein.

Pamoja na hayo, alimueleza haja ya kuwepo ushirikiano wa kutosha kwa askari wa barabarani pamoja na taasisi husika inayotoa leseni za udereva wa vyombo vya moto ili kuepusha ajali zisizo za lazima ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

Alimueleza mkuu huyo wa Jeshi la Polisi kuwa kumekuwepo ongezeko kubwa la ajaili za barabarani ambazo nyingi husababisha vifo, ulemavu wa viungo pamoja na hasara nyingine za mali, hivyo kuna haja ya kuchukuliwa hatua za makusudi katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

Naye IGP Sirro alitoa shukurani kwa Dk Shein na kupongeza kwa ushirikiano mkubwa linaoupata Jeshi hilo kutoka kwa wananchi na viongozi wote wa SMZ. Aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendeleza amani na utulivu huku akisisitiza kudumishwa kwa maslahi ya nchi.

IGP Sirro alimhakikishia Dk Shein kuwa hatua za makusudi zitachukuliwa kuhakikisha changamoto zilizopo kwa Jeshi la Polisi Zanzibar zinapatiwa ufumbuzi sambamba na kusimamia usalama wa barabarani

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *