Home / Habari Za Kitaifa / Askofu: Watanzania tumuunge mkono Rais Magufuli

Askofu: Watanzania tumuunge mkono Rais Magufuli

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Agustino Shao amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa hatua anazochukua, kurekebisha mambo muhimu kwa maendeleo ya taifa, licha ya kuwepo kwa changamoto katika kipindi cha mpito.

Askofu Shao alisema hayo jana wakati akihubiri katika Misa Takatifu iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Minara Miwili, ambapo Rais Magufuli aliungana na waumini wa Kanisa Katoliki, kusali Ibada ya Jumapili ya Dominika ya 28 ya mwaka A wa Kanisa.

Akitoa mfano wa nchi ya Zimbabwe, ambayo Rais Robert Mugabe aliamua kuchukua hatua za kupigania maslahi ya Wazimbabwe na sasa wananchi wa nchi hiyo wameanza kuzalisha bidhaa na kuziuza nje ya nchi, Askofu Shao alisema hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli kupambana na rushwa, kupigania rasilimali za Watanzania, kuimarisha nidhamu na uwajibikaji, kukabiliana na wizi na ubadhirifu wa mali za umma na kubana matumizi, zinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote.

“Hatutaweza kusema tunaimaliza rushwa wakati tunaendelea kuishi kwa kupata fedha ambazo hujazifanyia kazi, ni lazima tuishi machungu ya kuimaliza rushwa, ni lazima tuishi machungu ya kuweka uadilifu katika utendaji wetu, tusipoishi machungu hayo tutaishi dunia mbili, dunia ya rushwa na dunia ya kujenga uchumi na uadilifu wa Watanzania, tukubali kujikatalia ili tuweze kupata mazuri tuliyotaka,” alisema Askofu Shao.

Katika salamu zake baada ya kumalizika kwa Misa Takatifu, Rais Magufuli alimshukuru Askofu Shao kwa mahubiri yake na ameungana naye, kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali inachukua hatua za kupambana na rushwa na kulinda rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha wananchi wenyewe.

Rais Magufuli alisema hata Baba wa Taifa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye juzi alitimiza miaka 18 tangu afariki dunia, alipiga vita rushwa na alipigania rasilimali za nchi, hivyo alitaka Watanzania wote kuungana katika juhudi hizo.

Dk Magufuli ambaye aliongozana na mkewe, Mama Janeth, aliwashukuru Watanzania wote kwa maombi yao na alichangia Sh milioni moja kwa ajili ya kwaya ya kanisa hilo na Sh milioni tano kwa ajili ya maendeleo ya Kanisa.

Rais, ambaye alirejea jijini Dar es Salaam jana, alikuwa Zanzibar ambako juzi alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Wiki ya Vijana zilizofanyika katika Uwanja wa Amaan.

Kabla ya kuondoka Ikulu Zanzibar, Rais Magufuli alikula chakula cha mchana na wakimbizaji Mwenge wa Uhuru mwaka huu, walioongozwa na Amour Hamad Amour na kuwahakikishia kuwa Serikali itafanyia kazi taarifa ya Mwenge, waliyoiwasilisha kwake jana.

“Mlipokuwa mkikimbiza Mwenge wa Uhuru, nilikuwa nafuatilia miradi mliyokuwa mnatembelea na maelekezo mliyokuwa mkitoa, sehemu zote mlizobaini kuwepo kwa dosari ninawahakikishia kuwa tutazifuatilia na kuchukua hatua,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema kuwa anatambua uzalendo waliouonesha wakati wote wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru na amewasihi kuendeleza maadili na uzalendo huo kwa manufaa ya taifa.

Wakimbizaji Mwenge hao walimshukuru Rais Magufuli kwa heshima kubwa na upendo aliyowaonesha, kwa kupokea taarifa yao na kuahidi kuifanyia kazi na pia kuwaalika kula nao chakula cha mchana, kwa kuwa hii imekuwa ni historia ya kipekee kwa wakimbizaji Mwenge wa Uhuru nchini.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *