Makala

Mwanasaikolojia achambua sababu za mtu kujitoa uhai

KIFO cha mwanasayansi kikongwe wa Australia, David Goodall (104) aliyetimiza azma yake ya kujiua kwa msaada wa kuchomwa sindano katika hospitali moja nchini Uswisi, kimetajwa kutokana na sababu ya nane na ya mwisho ya nadharia ya saikolojia.

Akizungumzia sababu ya kikongwe huyo kuamua kumaliza uhai wake kwa msaada wa dawa, Mwanasaikolojia wa hapa nchini, Mkang’u Lyadunda anasema siyo jambo la kawaida, bali ni tatizo la kisaikolojia na linawakumba zaidi watu wenye umri mkubwa ambao mara nyingi hujaribu kuvuta picha ya maisha yao ya awali na kuona ama hawezi tena kufanya yale aliyoyafanya. Akielezea kwa undani, Lyadunda alisema kitaalamu hali hiyo inaitwa integrity against despair ambayo ni nadharia au hatua ya nane na ya mwisho kwenye masuala ya saikolojia ambapo huwapata watu wenye umri wa kuanzia miaka 65 na kuendelea ambao huanza kuwaza kama alitumia vizuri maisha yake akiwa na nguvu.

Lyadunda alisema kisaikolojia, binadamu anapofikisha umri huo huanza kujaribu kuvuta picha kuangalia kama alitimiza malengo yake akiwa na nguvu na iwapo akiona hakutimiza, basi huwaza kifo. Aidha, alisema pia anapovuta picha na kuona akiwa na nguvu alifanya yote aliyoyataka basi huona hakuna sababu ya kuendelea kuishi hivyo kinachofuata ni kifo. “Zipo sababu za mtu kuamua kufa sio kwamba ni jambo la kawaida, kitaalamu lazima kuna sababu na baadhi ni kama akiona hakutimiza wajibu wake akiwa na nguvu, anachodhani kinafaa ni kuamua kujiua, au alifanya yote na sasa hana cha kufanya kimebaki kifo,” anasema Lyadunda. Sababu nyingine za mtu mzee kuamua kufa ni kupatwa tatizo la sonona ambapo mhusika huwa na mawazo hasi na hatimaye anaona hakuna sababu ya kutafuta msaada wa kisaikolojia na jambo pekee ni kujiua.

Akioanisha sababu hizo za kisaikolojia na tukio la Goodall kuamua kumaliza uhai wake kwa msaada wa dawa, Lyadunda anasema limetokana na nadharia hiyo ya nane na ya mwisho ya nadharia ya kisaikolojia. Anasema mwanasayansi huyo awali alisema amekuwa akifanya kazi zake za kitafiti msituni na sasa hawezi tena kutokana na mwili wake kuchoka na macho kupoteza uoni wake na kwamba jambo hilo limemnyima furaha kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita. Mzee huyo alinukuriwa akisema: “Maisha yangu yaliyokuwa ya kufanya kazi za kitafiti yaani kuzunguka huko na huku, kwa sasa siwezi tena, kila ninachokitaka inabidi kusaidiwe tena kwa kusukumwa na baiskeli.” Goodall alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na kituo cha matangazo ya televisheni cha CCN mapema wiki hii kabla ya kujiua.

“Ninapenda kutembea tena kwenye misitu kuona vitu vilivyomo, natamani kusikia sauti za ndege, lakini siwezi tena macho hayaoni tena,” alisema kikongwe huyo aliyeacha watoto wanne na wake watatu. Lyadunda anasema kauli hizo za kikongwe huyo zinaonesha wazi kwamba alihitaji msaada wa kisaikolojia, ila hakuona sababu ya kutafuta na badala yake aliamua kutafuta msaada wa kujiua. Pia Lyadunda anasema sababu nyingine ya kikongwe huyo kuamua kujiua ni kujitenga, kwani alijiona kwa umri alionao hawezi tena kufanya chochote kama zamani, na ndiyo maana alipohojiwa na vyombo vya habari alisema alizoea maisha ya kufanya utafiti na kusikiliza sauti za ndege msituni, ila sasa hawezi na badala yake anasaidiwa na watu hata kuendeshwa kwenye baiskeli.

Ushauri Hata hivyo, mwanasaikolojia huyo anasema ni hatari kwa nchi kuruhusu uwepo wa sheria kama hiyo inayompa uhalali mtu kuamua kukatisha uhai wake. Anasema hiyo ni kwa sababu yapo matatizo yanayoweza kupatiwa suluhu kwa msaada wa wanasaikolojia. Akaongeza kwamba ni vyema watu wanapofikisha umri kuanzia miaka 60, ndugu wa karibu wawe wanazungumza nao na ikiwezekana wawatafutie wataalamu wa saikolojia ili wawashauri jinsi ya kuishi uzee mwema na siyo kufikiri kujiua. “Ndiyo maana utaona mtu akistaafu huwa haishi tena maisha marefu anakufa, ni kwa sababu huwa anaanza kutathmini maisha yake ya nyuma na kama hakutimiza malengo, huishia kukata tamaa na kuamua kujiua,” anasema Lyadunda.

Nchi zinazoruhusu kujiua Ingawa uamuzi wa kujiua ni mkubwa, lakini zipo baadhi ya nchi zimehalalisha uamuzi huo na baadhi yake ni Ubelgiji ambayo sheria hiyo ilianza kutumika Mei, 2002 na wanaotekeleza wengi ni wagonjwa wa saratani ambayo hufanyia kitendo hicho nyumbani. Canada ilihalalisha sheria hiyo mwaka 2015/16 kwa watu wote wanaohitaji kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea. Nchi nyingine ni Korea Kusini, Japan, Uholanzi, Uholanzi na Luxemburg ambayo imeruhusu ila ni lazima mtu apate kibali cha madaktari wawili na jopo la wataalamu. Nyingine ni Uswisi ambako Goodall aliamua kwenda kusitisha uhai wake na baadhi ya majimbo nchini Marekani kama vile Washington DC, Oregon, Montana, California na Visiwa vya Hawaii.

Aidha, Colombia imeanza kutumika sheria hiyo Desemba, 2014 kwa kuitaka Wizara ya Afya kutoa kibali hicho kwa wagonjwa mahututi kama wale wa saratani, figo, ini, Ukimwi na wa kutetemeka (Parkinson). Kikongwe Goodal alitimiza azma yake ya kujiua Mei 10, mwaka huu, alfajiri saa tisa na dakika 12 katika Kliniki ya Life Circle mjini Basel kwa kijidunga sindano yenye dawa aina ya lethal kwa msaada wa madaktari. Tukio hilo la kustaajabisha lilivuta hisia za watu duniani kote ambapo awali wiki mbili kabla ya kufanya uamuzi huo, alichangisha fedha Dola za Marekani 20,000 (takriban Sh milioni 44) zilizomsaidia kusafiri kwa ndege daraja la kwanza kutoka nyumbani kwake Perth, Australia kwenda Uswisi kutafuta msaada wa kukatisha uhai wake.

Uamuzi wa kusafiri kwenda Uswisi unatokana na nchi yake kutokuwa na sheria inayoruhusu au kuhalalisha mtu kujiua. Hata hivyo, Jimbo la Victoria nchini humo litaanza kutumia sheria hiyo mwakani. Awali, mwanasayansi huyo alifanya jaribio la kujiua nchini mwao, lakini ilishindikana na kujikuta hospitalini akipatiwa matibabu. Aliruhusiwa na hakufunguliwa mashtaka baada ya ripoti ya mtaalamu wa magonjwa ya akili kutoka.

Alisema uamuzi wake huo wa kujiua ni wa busara, ndiyo maana akaamua kusafiri kwenda Uswisi na kwamba akikamilisha azma yake hiyo ya kujiua. “Ninaamini kutakuwa na matokeo mazuri, nina furaha kwamba hatimaye ninachokitaka kitatimia kwa kutumia teknolojia ya euthanasia,” alisema Goodall mwanzoni mwa wiki hii. “Siogopi kifo ninakitamani na kimefika.” Kikongwe huyo alistaafu mwaka 1979 na enzi za uhai wake amehariri mfululizo wa vitabu 30 viitwavyo ‘Ecosystems of the World’, ambavyo vimeandikwa na watunzi zaidi ya 500. Mwaka 2016, alipewa Tuzo ya Heshima ya Australia.

Show More

komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close