Home / Habari Za Kitaifa / PACHA WA BUKOBA WAENDA KUTENGANISHWA

PACHA WA BUKOBA WAENDA KUTENGANISHWA

PACHA Almesia na Anisia Benardo walioungana wameondoka nchini jana chini ya jopo la madaktari kuelekea Saudi Arabia kwa upasuaji wa kuwatenganisha.

Daktari Bingwa wa Upasuaji Watoto, Zaituni Bokhari amesema kuwa ni matarajio yake kuwa upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao utafanikiwa.

“Kikubwa Watanzania wawaombee watoto hawa, Mungu akasimamie upasuaji wao ukafanikiwe na waweze kurejea nyumbani salama,” amesema Bokhari ambaye mwaka 2013 alikuwa miongoni mwa madaktari bingwa waliofanikisha upasuaji wa watoto pacha waliokuwa wameungana Eliud na Elikana wa mkoani Mbeya.

Watoto hao, Almesia na Anesia walizaliwa Januari 29, wilayani Misenyi, Bukoba, mkoani Kagera katika Kituo cha Masista cha St Theresa Omukajunguti Kata ya Kyaka na kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam mapema mwezi Februari, mwaka huu.

Baada ya kufika Muhimbili waliwekwa kwenye Wodi Maalumu ya Jengo la Watoto ya Magufuli, wakipatiwa matibabu ya awali kabla ya jana kupelekwa Saudia Arabia kwa matibabu.

Watoto hao wameungana eneo kubwa la kifuani na tumbo, lakini kila mmoja ana mfumo wake wa hewa. Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Bandar Abdullah Al – Hazani alilieleza gazeti hili kuwa watoto hao watafanyiwa upasuaji huo wa kuwatenganisha katika Hospitali ya Mfalme Abdulaziz Medical iliyopo Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, ambako kuna madaktari bingwa wa upasuaji.

Alisema mpango huo wa kufanikisha matibabu ya upasuaji wa kuwatenganisha pacha hao, umefanywa kwa ushirikiano wa ubalozi wa Saudi Arabia nchini chini ya Balozi wake, Mohamed Bin Mansour, uongozi wa Hospitali ya Muhimbili na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga.

Hospitali ya Mfalme Abdulaziz Medical huko Riyadh, ina uwezo mkubwa ikiwa na vifaa vya kisasa na vitanda 1,501 na ilianza shughuli zake Mei 1983. Mama wa pacha hao, Jonisia Jovitus (21) alisema:

“Nina hofu, Mungu asaidie nirudi na wanangu, ninaogopa sana, niombeeni. “Naomba Mungu asaidie hili lifanikiwe… ila walichoniambia ni kuwa wanangu wakifanikiwa kutenganishwa salama watakuwa walemavu, mmoja atakuwa na mguu mmoja na mwingine ana miguu miwili, lakini huo mmoja hauna nguvu umepooza. Ninachoomba kwa sasa ni kuwaona watoto wangu wako salama.”

Kwa upande wa Dk Bokhari akizungumzia sababu za pacha kuzaliwa wakiwa wameungana alisema kuwa hadi sasa hakuna sababu maalumu inayojulikana kisayansi.

Aliongeza kuwa pacha walioungana huwa ni matokeo ya kushindwa kukamilika kwa mchakato wa yai kugawanyika na hatimaye kila upande kuanza kujenga viungo vyake ili wapatikane pacha wanaofanana.

Mchakato huu hutakiwa kufanyika kati ya wiki ya tano na wiki ya nane ya ujauzito. Hata hivyo, kwa sababu ambazo hazijajulikana, mchakato huo hugoma kukamilika katika kipindi hicho na kusababisha kuzaliwa kwa pacha walioungana.

Alisema tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa kuna vihatarishi vinavyoweza kusababisha yai lishindwe kutengana sehemu mbili, kama inavyotakiwa na kutaja sababu hizo hatarishi kwa wazazi wote wawili kunywa pombe kupindukia, kuvuta sigara kupita kiasi, mtindo wa vyakula visivyofaa kama mafuta mengi, unene kupita kiasi na kutofanya mazoezi.

Kwa mujibu wa daktari huyo bingwa, tafiti zinaonesha kuwa tatizo la watoto pacha kuzaliwa wakiwa wameungana ni mara chache kutokea duniani ambapo kati ya kila watoto 100,000 wanaozaliwa, ni tukio moja huwa ni la pacha walioungana.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *