Home / Afya / WANAWAKE WATAKIWA KUNYONYESHA WATOTO MAZIWA YAO PEKEE

WANAWAKE WATAKIWA KUNYONYESHA WATOTO MAZIWA YAO PEKEE

WANAWAKE wametakiwa kunyonyesha watoto maziwa ya mama pekee bila kuwapa maji, kinywaji au chakula kingine katika kipindi cha miezi sita baada ya kuzaliwa kwao.

Pia wameambiwa kuwa watoto wanatakiwa kupewa dawa, chanjo na matibabu mengine kwa ushauri wa watoa huduma za afya mahali hapo. Ushauri huo ulitolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Chemba, Chrisantus Funda. Alisema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Watoto Duniani Agosti 7, 2018 iliyofanyika kitaifa wilayani humo.

“Watoto wanatakiwa kuanza kunyonya maziwa ya mama mapema katika kipindi kisichozidi saa moja baada ya mama kujifungua tu,” alisema. Alisema watoto wanatakiwa kuanzishiwa ulaji kama chakula cha nyongeza baada ya kufikisha miezi sita lakini izingatiwe na kina mama kuwa chakula kikuu cha watoto ni maziwa ya mama.

“Vyakula vya ziada ni vya asili ya nafaka, mizizi na ndizi zisizoiva, vyakula vya asili ya wanyama na mikunde, mboga, matunda, mafuta, sukari na asali kwa kiasi kidogo,” alisema. Alisema mama anatakiwa kumnyonyesha mtoto maziwa yake hadi atimize miezi 24 au zaidi kwani unyonyeshaji wa maziwa ya mama unaupatia nguvu mfumo wa ukuaji na maendeleo ya ufahamu na utambuzi (IQ).

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Ofisa Lishe wa World Vision Tanzania, Kanda ya Kati, Dk Salome Mtango alisema, akina baba wanatakiwa kuchangia na kuhakikisha kina mama wanapata chakula bora kwa ajili ya kutengeneza maziwa ya mama kunyonyesha. “Mama anatakiwa kula vizuri, kula chakula mchanganyiko na maji ili kupata chakula cha kutosha.

Hivyo katika kuhakikisha chakula kinapatikana kwa mama anayenyonyesha ni jukumu la familia nzima hasa baba,” alisema. Alisema akinamana wanatakiwa kupunguziwa kazi wakati wananyonyesha, hivyo akina baba wanatakiwa kuwasaidia wanawake kazi zao ili wanawake wapate nafasi ya kunyonyesha.

“Mama anayenyonyesha anatakiwa kupunguziwa maudhi yanayoletwa na jamii inayomzunguka akiwemo mume, familia, ndugu wa pande zote mbili pia,” alisema. Ofisa Lishe wa Wilaya ya Chemba, Faith Tema alisema wanawake wanatakiwa kuzingatia unyonyeshaji kwani takwimu zinaonesha kati ya watoto 10 ni sita tu ndio wananyonyesha maziwa ya mama pekee katika miezi hiyo sita.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Je wajua kwamba nguo za kubana huathiri ‘mbegu za kiume’?

Na Lucy R GreenScience fellow Kaptula ya ndani kama iliyovaliwa na Gary Lineker kwenye mechi …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *