Home / Habari Za Kitaifa / Machinga Kuondolewa Ubungo

Machinga Kuondolewa Ubungo

Serikali imeagiza wafanyabiashara ndogo maarufu ‘machinga’ kuondolewa eneo la Ubungo, Dar es Salaam, kupisha shughuli za ujenzi wa barabara za juu unaoendelea katika eneo hilo.

Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo na ujenzi wa daraja la juu eneo la Tazara.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe na Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuhakikisha wafanyabiashara hao wanaondolewa na kupelekwa kwenye maeneo yaliyoandaliwa kwa ajili yao.

Majaliwa alisema kuondolewa kwa wafanyabiashara hao, kutatoa nafasi kwa mkandarasi kutekeleza majukumu yake bila kikwazo na kukamilisha mradi huo kwa wakati uliokubalika.

Lakini, pia itasaidia kuondoa vitendo vya wizi wa vifaa vya ujenzi kutokana na mwingiliano kati ya wafanyakazi na watu wengine wasiohusika. Ujenzi huo wa daraja la ngazi tatu kwenye makutano ya Barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo, unatekelezwa na Kampuni ya ujenzi ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).

Daraja hilo litakuwa na urefu wa takribani mita 1,000 na njia sita. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Patrick Mfugale, alimweleza Waziri Mkuu kwamba ujenzi wa barabara hizo za juu, utakamilika ndani ya miezi 30 kuanzia Mei 22, 2017 mradi ulipoanza na utakamilika mwezi Juni 2020.

Mfugale amesema upanuzi wa madaraja mawili yaliyopo Barabara za Mandela na Sam Nujoma, yatakayosaidia kuchepusha magari wakati ujenzi unaendelea, yatakamilika mwezi Novemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa Tanroads, mradi huo unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 450, huku gharama za awali za mradi huo ni Sh bilioni 177.425 na mpaka sasa mkandarasi ameshalipwa Sh bilioni 42.401.

Daraja la juu Tazara Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa daraja la juu kwenye makutano ya Barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara, Waziri Mkuu alisema umefikia asilimia 98. Majaliwa alisema serikali imeridhika na kazi iliyofanyika mpaka sasa na ukaguzi alioufanya ni wa mwisho.

Alisema daraja hilo lenye urefu wa kilomita moja, litazinduliwa na Rais John Magufuli mwezi Oktoba mwaka huu.

Alisema kukamilika kwa daraja hilo, kutafanya magari yanayotoka na kwenda upande wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kutosimama kwenye makutano hayo.

Hatua hiyo itapunguza muda wa safari katika barabara hiyo kwa wastani wa asilimia 50 kutoka wastani wa dakika 45 za sasa hadi kufikia dakika 20. Kwa mujibu wa Tanroads, mradi huo umejengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa fedha za Japan Yen bilioni 4.847 sawa na Sh bilioni 92.093.

Serikali ya Tanzania imechangia Sh bilioni 8.46 kwa ajili ya kulipa fidia, uondoshaji wa miundombinu ya umeme, maji, simu, gesi na tozo mbalimbali za kodi.

Kuhusu nafasi ya katikati iliyoachwa kati ya daraja na daraja eneo la chini, Waziri Mkuu alisema itatumika kwa ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendokasi kutoka katikati ya Jiji kwenda Gongo la Mboto na Pugu. Ujenzi wa daraja hilo la juu eneo la Tazara, ulianza Oktoba 15, 2015 na utakamilika Oktoba 31 mwaka huu na litakuwa likiitwa ‘Mfugale Flyover’.

Mwonekano wa barabara utakavyokuwa Ubungo Ngazi ya kwanza ya ujenzi huo, unahusu barabara ya chini kwa ajili ya kupitisha magari yanayotoka na kwenda upande wa Kimara na katikati ya Jiji kwa kutumia barabara ya Morogoro na mabasi ya mwendo kasi. Kwa mujibu wa Tanroads, ngazi ya pili itahusu ujenzi wa barabara za juu zenye kimo cha mita saba kutoka usawa wa barabara ya sasa.

Barabara hii itapitisha magari yanayopinda kulia kutokea pande zote za barabara hizo ili yavuke makutano ya barabara yakiwa na taa za awamu mbili badala ya awamu nne zilizopo sasa.

Katika ngazi hiyo, kila barabara itakuwa na mwanzo wa mwinuko (ramp), utakayoyawezesha magari kufika sehemu ya juu na kushuka kwenda sehemu nyingine.

Kuanzia mwanzo wa mwinuko wa barabara ya kutokea Kimara kuelekea Buguruni, itakuwa na urefu wa mita 580, wakati mwanzo wa mwinuko wa barabara ya kutokea mjini (Barabara ya Morogoro) kuelekea Mwenge, itakuwa na urefu wa mita 460.

Kuhusu upande wa mwanzo wa mwinuko wa barabara ya kutokea Mwenge kuelekea Kimara, itakuwa na urefu wa mita 590, wakati mwanzo wa mwinuko wa barabara ya kutokea Buguruni kuelekea mjini (Barabara ya Morogoro) itakuwa na urefu wa mita 380.

Wakati ngazi ya tatu ya barabara hiyo, itakuwa na kimo cha mita 14 kutoka barabara inayotumika sasa kwa ajili ya magari yanayokwenda na kutoka pande za Mwenge na Buguruni. Magari ya pande hizo mbili, hayatasimama katika makutano hayo.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *