Home / Habari Za Kitaifa / Utata Kuondolewa Chaneli Zisizolipiwa

Utata Kuondolewa Chaneli Zisizolipiwa

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeombwa kuwaelimisha Watanzania, kuhusu kuondolewa kwa chaneli zisizolipiwa kwenye visimbuzi vinavyotoa maudhui kwa malipo.

Ombi hilo lilitolewa na wadau wa habari nchini na wanasheria kutokana na ukweli kuwa pamoja na Kanuni na Masharti ya Leseni kuweka zuio la visimbuzi hivyo kurusha chaneli zisizolipiwa, bado kuna mjadala mkubwa kuhusu utekelezaji wa suala hilo.

TCRA pia imetakiwa kuhakikisha inaviwezesha visimbuzi vinavyorusha chaneli zisizolipiwa ili viweze kufikia wananchi wengi, kwani kwa sasa vingi bado soko lake halifahamiki.

Wadau hao waliyasema hayo katika semina ya siku moja ya kujadili haki ya kupata taarifa, iliyowashirikisha waandishi wa habari, TCRA na wanasheria, iliyoandaliwa na taasisi ya Internews kwa ufadhili wa shirika la USAID.

Akizungumza katika semina hiyo, Wakili Mwandamizi kutoka Victory Attorneys, Samwel Gerald amesema bado elimu inahitajika kwa wananchi kuhusu suala hilo ili kuondoa sintofahamu mitaani.

“Katiba yetu iko wazi kuhusu haki ya mwananchi kupata taarifa. Suala hili limezua mjadala sana ingawa sheria iko wazi,” alisema.

Amesema moja ya majukumu ya mamlaka hiyo ni kuufahamisha umma kuhusu majukumu yake, lakini katika suala hilo la kuondoa chaneli zisizolipiwa, bado mambo mengi muhimu wananchi hawafahamu.

Awali, akielezea Sheria ya TCRA ya mwaka 2003, Mwanasheria kutoka Mahakama Kuu, Flodius Mutungi, amesema sheria imeweka bayana masharti ya leseni kwa kampuni za ving’amuzi. Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, kuna leseni za aina mbili ambazo ni leseni inayoruhusu king’amuzi kurusha chaneli zisizolipiwa na leseni inayoruhusu visimbuzi kurusha chaneli zinazolipiwa.

“Sheria hizo ziko wazi na zimeweka masharti ya kutoingiliana. Adhabu kwa anayekiuka ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja,” alifafanua.

Mhandisi kutoka TCRA, Joel Chacha amesema, kwa mujibu wa kanuni mpya zilizotoka mwaka huu, kisimbuzi kinachorusha chaneli zinazolipiwa maudhui, haiziruhusiwi kurusha matangazo ya ndani.

“TCRA ilifanya mchakato wa kutafuta watoa huduma ya chaneli zisizolipiwa kwa kushirikisha wadau, ambao walijenga miundombinu ardhini. Sisi hawa tupo nao na tunafanyanao kazi kwa karibu,” amesema.

Hata hivyo, Mshauri Mwandamizi wa Twaweza alisema visimbuzi vinavyotumiwa na TCRA kwa sasa bado soko lake halifahamiki, lakini pia hali ilivyo mtaani kuhusu suala hili ina mkanganyiko.

“Mile sielewi ni kwamba sasa nikitaka kupata maudhui yote yanayolipiwa na yasiyolipiwa inabidi niwe na dikoda zaidi ya moja? amehoji.

Mhariri Mtendaji wa Nukta Africa Ltd, Nuzulack Dausen amesema alielezea namna kuondolewa kwa chaneli hizo, kunavyowaathiri wananchi na uchumi kwa ujumla.

Amesema kitendo cha wananchi kukosa taarifa za ndani kutoka vyanzo mbalimbali, kinawanyima fursa ya kupambanua na kuchambua mambo, lakini pia wadau au wafanyabiashara wanakosa taarifa za kuwajenga zaidi kiuchumi.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *