Home / Habari Za Kitaifa / Standard Chartered Kutoa Trilioni 3.3/- za SGR

Standard Chartered Kutoa Trilioni 3.3/- za SGR

Benki ya Standard Chartered Group imekubali kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa Dola za Marekani bilioni 1.46 sawa na zaidi ya Sh trilioni 3.3 kwa ajili ya kujenga kipande cha Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kuanzia Morogoro hadi Makutupora, mkoani Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameyasema hayo alipokutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bill Winters, jijini Dar es Salaam.

“Tunajenga reli hiyo ya kisasa kutoka Dar es Salaam – Morogoro hadi Makutupora ambazo ni awamu mbili, pia tutajenga reli hiyo kuelekea Isaka mpaka Mwanza na baadaye Rusumo ambapo wenzetu wa Rwanda, tutasaidiana, wao watajenga reli hiyo kutoka Rusumo hadi Kigali,”amesema.

Dk. Mpango amemweleza kiongozi huyo wa Standard Chartered Group anayeongoza benki hiyo kwenye nchi zaidi ya 60 duniani, kuhusu vipaumbele vikubwa vya nchi ikiwemo kuboresha Kampuni ya Ndege Tanzania(ATCL) na ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Mto Rufiji.

Amesema Tanzania ni ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikitanguliwa na Brazil, lakini inapokea watalii wasiozidi milioni mbili kwa mwaka jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka ili sekta hiyo ichangie uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa kupitia fedha za kigeni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Group, Bill Winters, ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kiuchumi na kwamba benki yake itatoa mkopo huo na kuahidi kuwa balozi wa kuelezea mafanikio makubwa ya kiuchumi ya Tanzania kwa wadau wengine.

Ameahidi kuzishawishi taasisi nyingine za fedha ulimwenguni kuangalia uwezekano wa kuunga mkono jitihada hizo ambazo mwisho wake wanufaika wakubwa watakuwa ni wananchi wote wa Tanzania kwa ujumla.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *