Home / Michezo / Bilionea mmiliki wa Leicester City Vichai Srivaddhanaprabha athibitishwa kufariki dunia ajali ya helikopta Uingereza

Bilionea mmiliki wa Leicester City Vichai Srivaddhanaprabha athibitishwa kufariki dunia ajali ya helikopta Uingereza

Bilionea mmiliki wa klabu ya Leicester City FC amethibitishwa kuwa miongoni mwa watu waliofariki katika ajali ya helikopta karibu na uwanja wa klabu hiyo Jumamosi.

Klabu hiyo imethibitisha kuwa Vichai Srivaddhanaprabha, 61, kutoka Thailand, wafanyakazi wawili wake, rubani na abiria mmoja walifariki baada ya ndege hiyo kuanguka mwendo wa saa mbili unusu usiku.

Bilionea Mmarekani David Rockefeller afariki

Mambo matano unayoyahitaji kuwa bilionea

Walioshuhudia wanasema ndege hiyo ilikuwa tu imemaliza kuondoka uwanjani pale ilipoanza kuyumba na kuanguka na kuwaka moto.

Maelfu ya watu wameweka maua na skafu za ukumbusho nje ya uwanja wa King Power, na pia ujumbe wa kuwafariji waliofiwa.

Polisi wa Leicestershire wamesema waliofariki duniani wanaaminika kuwa:

  • Mmiliki wa Leicester Vichai Srivaddhanaprabha
  • Wafanyakazi wake wawili, Nursara Suknamai na Kaveporn Punpare
  • Rubani Eric Swaffer na mpenzi wake Izabela Roza Lechowicz

(Kushoto kwenda Kulia) Izabela Roza Lechowicz, Eric Swaffer, Nursara Suknamai na Kaveporn Punpare wote walifariki katika ajali hiyo

Bi Swaffer alikuwa na uzoefu wa miaka 20 akiendesha ndege za kibinafsi na helikopta.

Katika taaluma yake, alikuwa ameendesha helikopta zinazotumiwa na vyombo vya habari kufanya matangazo ya moja kwa moja.

Miongoni mwa mashirika aliyoyafanyia kazi ni Channel 4 katika kipindi chao cha The Big Breakfast na pia amewafi kufanyia kazi kipindi cha Virgin Radio.

Lucie Morris-Marr, rafiki yake Swafer, amesema alikuwa rubani mzoefu sana na bila shaka angefanya kila aliwezalo kuzuia ajali hiyo.

Ameongeza kwamba alikuwa mtu mcheshi ambaye alikuwa kwenye mapenzi na Bi Lechowicz ambaye walikuwa wanafanya kazi naye.

“Sio watu wengi huamka na kusafiri na wapenzi wao, wakisafiri maeneo mbalimbali duniani na baadhi ya kifahari,” alisema.

Wawili hao wapenzi walikuwa marubani na walikuwa wakiishi pamoja Camberley, Surrey.

Bi Lechowicz alihamia Uingereza kutoka Poland 1997.

Maua na karatasi zenye salamu za rambirambi vimewekwa nje ya uwanja na mashabiki wa Leicester City

Srivaddhanaprabha alikuwa nani?

Bilionea Srivaddhanaprabha, 60, alikuwa ameoa na kujaliwa watoto wanne.

Alinunua Leicester City kwa £39m mwaka 2010 na akawasaidia kulipa madeni kisha kupanda ngazi hadi kucheza ligi kuu miaka minne baadaye.

Chini ya umiliki wake, klabu hiyo ilishinda taji la Ligi ya Premia 2016 baada ya kuanza msimu ikiwa haipigiwi upatu.

Srivaddhanaprabha alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya maduka yasiyotoza kodi ya King Power International Group ambapo ndipo jina la uwanja wa Leicester linatoka, na pia jina la mdhamini kwenye jezi zao.

Utajiri wake unakadiriwa kuwa $3.8bn (£2.9bn), na anakadiriwa na Forbes kuwa mtu wa nne kwa utajiri Thailand.

Ingawa alionekana kwenye mechi za Leicester, alikuwa mtu msiri sana na ilikuwa nadra kwake kufanya mahojiano na wanahabari.

Rambirambi

Kupitia taarifa, Leicester City imesema fikira za klabu hiyo zimo kwa “familia ya Srivaddhanaprabha na familia za wote waliokuwa kwenye ndege hiyo kwa msiba huo.”

Klabu hiyo imemweleza Srivaddhanaprabha kwamba “mtu mkarimu, mwema na ambaye maisha yake yalitawaliwa na upendo wake kwa familia yake na watu aliowaongoza.”

“Leicester City ilikuwa familia chini ya uongozi wake. Tutaomboleza kifo chake kama familia na kuendeleza juhudi za kutimiza ndoto yake kwa klabu hii ambayo sasa atakumbukwa kwa mchango wake.”

Kitabu cha kutoa rambirambi kitawekwa kwenye uwanja wa King Power kuanzia kesho Jumanne.

Mechi iliyokuwa inafuata ya klabu hiyo dhidi ya Southampton katika Kombe la EFL ambayo ilipangiwa kuchezwa Jumanne sasa imeahirishwa.

Uwanja wa Wembley uliangaza rangi za klabu ya Leicester

Leicester walikuwa wametoka sare ya bao 1-1 dhidi ya West Ham kwenye uwanja wa King Power huku mechi ikikamilika saa moja kabla ya helikopta hiyo kupaa kutoka uwanjani.

Walioshuhudia walisema waliiona ndege hiyo ikiondoka uwanjani kabla ya kupoteza mwelekeo na kudondoka kutoka angani huku wengine wakisema kuwa waliona moto mkubwa wakati ilianguka.

Kipa wa Leicester Kasper Schmeichel, ambaye walioshuhudia wanasema alikimbia kutoka uwanjani kuelekea eneo ambalo ndege hiyo ilianguka, amesema Srivaddhanaprabha atakumbukwa kama mtu “aliyebadilisha kandanda daima.”

“Siamini kwamba haya yanatokea. Nimesikitika sana na kuvunjika moyo,” ameongeza.

Nahodha wa klabu Wes Morgan ameandika kwenye Twitter ykwamba amejawa na majonzi kutokana na “taarifa kuhusu mwenyekiti wetu. Mtu aliyependwa na kuenziwa na kila mtu hapa lcfc.”

Mkuu wa Ligi ya Premia Richard Scudamore amesema: “Vichai alikuwa mwanamume aliyeshiriki katika mchezo huu kwa ustaarabu na ucheshi, na tutamkosa sana.

“Kazi aliyoifanya kwa Leicester – klabu na jiji – itakumbukwa daima.”

Klabu za Paris Saint-Germain, Inter Milan, West Ham United, Tottenham Hotspur, Nottingham Forest na Swansea City ni miongoni mwa zilizotuma salamu za rambirambi.

Picha ya Vichai Srivaddhanaprabha imewekwa miongoni mwa maua na karatasi zenye ujumbe nje ya uwanja

Polisi wa Leicestershire wamethibitisha kwamba hakuna watu wengine waliojeruhiwa kwenye mkasa huo, na kwamba uchunguzi umeanzishwa.

Helikopta hiyo ilianguka katika eneo la maegesho ambalo halikuwa linatumika lakini ilikuwa hatua chache kutoka kwenye majengo na maeneo yaliyokuwa na magari.

Afisa wa polisi Steve Potter amesema ingawa maafisa walifika mara moja eneo la mkasa, hawakufanikiwa kwa haraka kuuzima moto na kuwaokoa waliokuwa ndani.

“Licha ya juhudi zetu, hakukuwa na manusura.”

Potter amesema uchunguzi utachukua siku kadha.

Watu watano, akiwemo mmiliki wa Leicester, walifariki kwenye ajali hiyo

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Nyota wa Afrika wamkumbuka mmiliki wa Leicester City Vichai Srivaddhanaprabha

Riyad Mahrez (kushoto) ni mmoja ya walitoa heshima zao kwa Vichai Srivaddhanaprabha Wachezaji wa Kiafrika …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *