Habari Za KitaifaMakala

Sheikh Kishk awaongoza maelfu ya Waislamu katika Uchangiaji wa Damu

WATANZANIA wamehimizwa kuwajengea watoto utamaduni wa kushiriki katika shughuli za kijamii, ikiwemo kuchangia damu, kusafisha maeneo ya kijamii kama vile hospitali na kuhudumia wagonjwa.

Ushauri huo ulitolewa jana katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki, alipopokea matembezi ya hisani yaliyofanywa na Waislamu wa Wilaya ya Temeke.

Matembezi hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Alhikima Foundation kwa kushirikiana na Jumuiya ya Waislamu ya Kuhimiza Tabia Njema (Jamiiatul Ahlaaqil Islamiyya – JAI) yalilenga kutoa damu kwa wagonjwa, kusafisha mazingira ya hospitali ya Temeke, kuhudumia wagonjwa na kuwaombea dua pamoja na kuombea amani ya Tanzania.

“Nimefurahi sana kuona mmeshirikisha vijana wadogo walioko shule katika shughuli hii. Ni muhimu sana kwa jamii kuwaandaa vijana kupenda kufanya shughuli kama hizi za kijamii. Ninashukuru pia kuona namna akina mama wengi walivyokuja pia katika jambo hili,” alisema.

Alihimiza pia taasisi zingine za dini na Watanzania kwa ujuma kuiombea nchi yetu amani na kumwombea Rais John Magufuli atekeleze majumu yake ya kuongoza nchi kwa ufanisi.

Alisema siku zote wagonjwa wana mahitaji mengi yakiwemo ya damu na misaada mingine ikiwemo kusafishwa na hivyo akazitaka taasisi za Alhikma na JAI kudumisha utamaduni wa kusaidia na kuhudumia wagonjwa.

Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, alizishauri taasisi zingine kuiga mfano uliofanywa na Alhikma Foundation na JAI jana na kwamba yeye yuko tayari muda wote kutoa ushirikiano wake.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Dk Amaan Malima, alizishukuru taasisi zilizoandaa shughuli hiyo akifafanua kwamba muda wote wagonjwa na hospitali huwa na mahitai haya na yale.

“Kuchangia damu ni jambo jema sana kwa sababu huwezi kujua hata wewe unayetoa damu leo utaihitaji lini. Wala usione ajabu leo ukatoa damu kisha kesho na wewe ukahitaji kupewa damu.”

Mkurugenzi wa Alhikma Foundation, Shehe Nurdin Kishki, alisema kwamba matembezi hayo ya hisani ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 tangu taasisi hiyo ilipoanzisha mashindano ya Kurani.

Kishki ambaye pia ni mhubiri wa dini ya Kiislamu wa Kimataifa alisema Mashindano ya Kuran ya Afrika yanayotayarishwa na taasisi hiyo kwa mwaka huu yanatarajiwa kufayika Jumapili ya Mei 19. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: ‘Ukitaka dunia, shikamana na Kuran na ukitaka ahera shikamana na Kuran.’

Mbali na kuendesha mashindano ya kuhifadhi kurani, taasisi hiyo inamiliki shule ya chekechea, shule ya msingi, shule ya sekondari ya wasichana na shule ya sekondari ya wavulana. Wanafunzi wote wa shule hizo na walimu wao walishiriki pia matembezi hayo jana.

Awali, Shehe Kishki aliomba dua maalimu kwa ajili ya amani ya Tanzania dhidi ya wasioitakia mema, kisha akamwomba Mwenyezi Mungu amfanyie wepesi Rais John Magufuli katika uongozi wake. Shehe huyo pia aliwaombea dua wagonjwa wote katika hospitali ya Temeke na zingine nchini, Mwenyezi Mungu awaponye.

Mbali na kuchangia damu, Waislamu waliojumuika hospitalini hapo jana wakiweko wanafunzi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 1,300, walisafisha mazingira ya hospitali, kuogesha wagonjwa waliohitaji msaada huo huku wakipita mawodini kuwaombea dua.

Kadhalika waligawa vinywaji baridi, maji, buskuti na zawadi mbali kwa wagonjwa huku hospitali ikunufaika na vifaa mbalimbali vya kufanyia usafi. Watu zaidi ya 300 walitarajiwa kutoa damu jana.

Sheikh Nurdeen Kishk, Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation akiwa katika zoezi la kutoa damu, Pamoja na mwenyekiti wa JAI Taifa Sheikh Yahya Tatehe.

Waumini wa Kiislamu wakiwa katika zoezi la utoaji wa damu
Hizi ni miongoni wa uniti za damu zilitolewa na Waumini wa Kiislamu.
Waumini wa Kiislamu wakiwa katika foleni ya zoezi la utoaji wa damu
Hawa ni Miongoni mwa waumini wa kiislam walioitikia wito wa Al-Hikma na JAI katika zoezi la uchangiaji damu.

Hawa ni Miongoni mwa waumini wa kiislam wa kike walioitikia wito wa Al-Hikma na JAI katika zoezi la uchangiaji damu.

Sheikh Nurdeen Kishk, Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation akiwa katika zoezi la Usafi, Pamoja na Katibu wa JAI Taifa Sheikh Saad Ahmed Salim.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki, alipopokea matembezi ya hisani yaliyofanywa na Waislamu wa Wilaya ya Temeke

Sheikh Nurdeen Kishk Mkurugenzi wa Taasisi ya Al-Hikma Foundation akiwa katika zoezi la usafi katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke D.S.M Tanzania, siku ya tarehe 9/3/2019

Na Hamisi Kibari

Show More

komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close