Habari Za Kitaifa

BINGWA WA MAPISHI ANAYETIKISA DUNIA

“ILIKUWA Oktoba 28, mwaka huu, siku nilipoondoka nchini kuelekea Marekani katika jiji la Orange Beach, ambapo niliaga vizuri nikijua wazi kuwa nimebeba dhamana ya Taifa ili kuonesha dunia kuwa Tanzania kuna wapishi bora.

“Novemba 2, nilifika rasmi na kwa heshima ya Tanzania nilipokewa na mtawala wa jiji hilo ambalo ni eneo maarufu kwa masuala ya michezo, wakijivunia kuwa na fukwe ambazo zimekuwa zikiwaingizia fedha kutokana na biashara mbalimbali huku pia nikipewa zawadi maalumu ya kupigiwa makofi ya furaha pale nilipojitambulisha natoka Tanzania”.

Hayo ni maneno ya Fred Uisso (56) baba wa watoto watatu na mke mmoja ambaye ni Mtanzania pekee aliyeshika namba nne katika mashindano ya mapishi duniani ‘World Food Championship’ lililofanyika Marekani na kuwashirikisha washiriki 458 kutoka nchi 17 duniani, akiwa ni Mwafrika pekee aliyeingia fainali kati ya wapishi 21.

Akizungumzia mashindano hayo, Uisso ambaye pia aliwahi kuwa mwalimu wa shule ya msingi anasema yalifanyika katika eneo la Orange Beach, ambalo wakazi wake hulitumia kwa matukio mbalimbali, ikiwemo upishi wa vyakula mbalimbali hususan vinavyotokana na viumbe wa baharini (sea foods) na ni mara ya kwanza kwa mashindano hayo kufanyika katika jiji hilo.

Anasema kutokana na wakazi wa eneo hilo kutumia vyema fukwe za bahari, hujikuta wakiingiza watalii kwa wingi na takribani watalii milioni sita huingia eneo hilo kwa mwaka.

Uisso anasema shindano la kwanza alitengeneza nyama ijulikanayo kama steki ambayo imepata heshima kubwa katika jiji hilo kutokana na kuwa na muonekano wa ramani ya Afrika ikionekana kulala katika bahari huku harufu nzuri ikiwasumbua wakazi wa eneo hilo.

Anasema mke wake ndiye muonjaji wa ladha ya vyakula vyake na kwamba alishawahi kupika steki yenye umbo la ramani ya Afrika na mkewe alimshauri kuiweka vizuri ramani hiyo ili iweze kuonekana kwa uzuri zaidi, hivyo alivyokuwa kwenye shindano alikumbuka maelekezo hayo na alitengeneza.

“Hata hivyo mbali na steki ile kuwa na muonekano mzuri haikufika mbele, wengi nilioshiriki nao walikuwa na wasifu (CV) kubwa wakati nikiwa bado mchanga lakini sikukata tamaa,” anasema Uisso.

Anasema katika shindano la pili walitakiwa kutengeneza chakula wanachokipenda kwa muda wa dakika 45 ambapo pia alitengeneza steki akiweka kamba ndani yake ambayo pia ilipendeza na katika hatua ya pili, alitakiwa kutengeneza chakula chochote lakini kwa kutumia jibini na kiwe tayari ndani ya dakika 20.

Uisso anasema hatua nyingine ilikuwa ni kumiliki jiko kwa dakika nane akitakiwa kumenya, kubandua na kutoa utumbo kwa chaza (oyster) ambapo alitakiwa kukamilisha dakika nane na kila mpishi aliweza kufanikisha sita akiwemo yeye.

“Hata nilipokuwa hapa nchini sikufanikiwa kubandua magamba ya chaza na hiyo ilikuwa ni mara yangu ya kwanza ambapo nikiwa nasubiri zamu yangu katika jiko langu walifika wanafunzi kutoka Chuo cha Mississippi kwa ajili ya kuona Mwafrika katika shindano hilo,” anasema Uisso na kuongeza kuwa aliwaeleza wanafunzi hao kuwa hajawahi kubandua maganda ya chaza ambapo mmoja wao alimfungulia simu na kumuonesha ndipo alipopata mwanga.

Mpishi huyo anasema anajutia kutokumbuka kupika hata ugali na mchicha kwa kuwa mmoja wa washindi wa shindano hilo kutoka Vietnam alipika chakula cha kwao akizungushia vyombo vya kupakulia vya majani huku kikinukia.

Aidha anasema jambo ambalo hatoweza kulisahau katika mashindano hayo ni pale alipopata punguzo la asilimia 50 kutoka katika hoteli aliyokuwa akikaa, hasa baada ya kuomba kufanya mazoezi ya kupika wakati akisubiri siku ya mashindano ambapo harufu ya chakula iliwavutia watalii wengi waliokuwa wakiishi katika hoteli hiyo ambayo ilikuwa haipiki vyakula.

“Siku ya kuondoka nilikuta nimewekewa ramani ya Tanzania ndani ya chumba changu kwa lengo la kunishukuru na nilipokwenda kusaini kuwa ninaondoka ndipo nilipokuta nimepewa ofa hiyo ya punguzo la asilimia 50,” anasema na kuongeza kuwa amekuwa akisifiwa katika Jiji la Orange Beach kwa kupeleka ladha ya kipekee ya chakula.

Uisso anasema katika jimbo hilo jambo ambalo hatoweza kulisahau ni pamoja na kutowaona askari Polisi au askari wa Usalama Barabarani katika maeneo mbalimbali ambapo wananchi wamekuwa wakijiongoza na kujisimamia wenyewe.

Anasema kama asingekwenda na muda wa mashindano asingeweza kushiriki kwa kuwa wapishi wengine kutoka nchi nyingine waliingia wakiwa na wasaidizi wao wawili ama watatu huku yeye akiwa peke yake.

Uisso anasema pamoja na safari yake ya ushindi kufikia hapo, bado ana nia ya kuingia tena katika mashindano hayo huku akiipongeza sana Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kutokana na ushirikiano waliouonesha, ikiwa pia ni pamoja na kumtembelea katika mgahawa wake wa Afrikando uliopo Kinondoni kisha kumuandikia barua na kumkabidhi bendera ya Tanzania.

Hata hivyo, Uisso anailalamikia safari yake ya ushindi kukosa ushirikiano hata wa wapishi wenzake ambapo amejitosa peke yake huku wakijitokeza watu binafsi kumdhamini akiwemo Mtanzania anayeishi Marekani, Deogratius Ngowi aliyediriki kuacha kazi zake kwa siku 10 na kushiriki hatua kwa hatua na kumchangia kwa kiwango kikubwa, ikiwemo pia gharama zake za hotelini. Mbali na kushika nafasi ya nne, Uisso anasema imempa faraja kubwa na anaishauri serikali kuwekeza zaidi katika maeneo ya fukwe za bahari kwa kuwa zinaonekana kuwa na faida kubwa.

“Kwa nchi za wenzetu, mapishi ni moja ya kivutio cha utalii… kweli naishangaa Tanzania kutotumia fukwe tulizo nazo ili zitumike kwa ajili ya kushirikisha watu katika mashindano ya upishi wa vyakula mbalimbali, jambo ambalo litasaidia kuongeza kipato pamoja na kuwaleta watalii pia,” anasema Uisso ambaye ni mara yake ya kwanza kushiriki katika mashindano hayo ambayo ni ya tano.

Anasema kuanzia Februari mwakani, ana mkakati wa kuanzisha Chuo cha Mapishi kupitia mtandao ambacho kitatoa mafunzo kwa bei nafuu, lengo likiwa ni kuinua eneo hilo ambalo ni moja ya kivutio cha utalii nchini. Uisso anasema pia ana mpango wa kutoa mafunzo ya moja kwa moja kupitia mitandao mbalimbali yanayohusu upishi kwa watoto wanaoanzia miaka 10 hadi 11 na kuendelea lengo likiwa ni kuwaandaa kuwa wapishi wakuu wa vizazi vijavyo.

Kuhusu kuanzisha chuo, anasema wapo Watanzania wengi ambao hushindwa kumudu gharama za kusomea mapishi, lakini kupitia chuo chake anataka kila mmoja atakayekuwa na nia ya kujifunza anufaike na kwamba atatoza kwa bei ya kawaida.

Kupitia chuo hicho ataweza kuwajenga na kuwaimarisha wapishi wa kujitegemea, lengo ikiwa ni kuikuza sanaa hiyo ambayo kwa Tanzania haijatumika ipasavyo.

Kuhusu kuwafundisha watoto anasema alipokuwa katika mashindano hayo, alibaini nchi nyingine huwaandaa watoto wadogo kuanzia miaka 10 na kuendelea kuja kuwa wapishi wakuu wa baadaye, jambo ambalo aliona ni jema kulifanyia kazi nchini.

Kwa Chama cha Wapishi anasema ni chama kinachoongozwa na watu kutoka nje ya nchi ambapo hawakuweza kutoa msaada kwake wakati alipouhitaji ili kushiriki katika mashindano hayo, kama nia ya kuiinua tasnia ya upishi nchini.

Alishiriki akiwa amebeba dhamana ya Taifa na aliweza kufanya mambo mengi ambayo hata kwa washiriki wengine ilikuwa ni funzo kwa kuwa hawakuwa wameyaona mashindano hayo kama yana manufaa na anawasihi wapishi nchini kuungana na kuwa na sauti moja itakayokuwa na manufaa nchini.

Kuhusu safari yake ya mapishi anasema alianzia mkoani Morogoro eneo la Mikumi mwaka 1979, akifundishwa na mpishi mkuu moja kwa moja na baada ya hapo aliiacha kazi hiyo na kwenda kusomea ualimu lakini mwaka 2012 alianza rasmi kazi ya mapishi.

Hata hivyo, anasema mbali na kusomea ualimu aliufanya kwa miezi sita pekee na kuacha kwa kuwa hakuweza kupata maslahi aliyoyataka ambapo pia alisomea utawala katika biashara (business management) na baadaye kuiacha na 2012 ndipo aliporudi katika mapishi na kufanikiwa kuanzisha mgahawa wa Afrikando.

Mkewe Monica, anasema amekuwa akisaidiana na mumewe pale inapobidi na amekuwa akimtia moyo kwa kuwa wanaamini kwamba wanatafuta maisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Geofrey Tengeneza anasema bodi hiyo inampongeza Uisso kutokana na kubeba dhamana kubwa katika kuiwakilisha nchi vizuri.

Mchakato wa shindano hilo ulikuwa na washindani wengi na Tanzania inajivunia kuwa na mpishi bora aliyeweza kushika namba nne katika upishi ambapo ni moja ya kivutio cha utalii wa kitamaduni.

“Ameitangaza nchi katika mapishi na utalii pia, hivyo watalii watakuja kuona na kuonja ladha ya vyakula vya kwetu na wengine kujifunza hata utamaduni wetu, kwa hakika ameitendea haki nchi yetu,” anasema Tengeneza.

SOURCE HABARI LEO.

Show More

komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close