Home / Habari Za Kitaifa / KAMPUNI ZATEKELEZA AGIZO LA NDIKILO.

KAMPUNI ZATEKELEZA AGIZO LA NDIKILO.

HATIMAYE baada ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kulitaka Jeshi la Polisi kuzifungulia mashtaka kampuni mbili za Alpha Choice Ltd na Kaasal Commodities Ltd kwa kushindwa kuwalipa wakulima wa zao la korosho kiasi cha Sh bilioni 5.7, kampuni moja imelipa huku nyingine ikitoa kiasi cha fedha.

Kampuni iliyolipa deni lake ni Alpha Choice Ltd ambayo ilikuwa ikidaiwa kiasi cha Sh 4,202, 514, 402 huku Kampuni ya Kaasal Commodities Ltd ikitoa kiasi cha Sh 342,200,768 na kubakiza deni la Sh 1,298,407,520. Awali ilikuwa ikidaiwa Sh 1,591,608,288.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na mkuu wa mkoa wa Pwani, deni hilo lililobaki waliahidi kulilipa ifikapo Desemba 19, mwaka huu.

Ndikilo alisema kampuni hizo zilifunguliwa mashtaka ya kukiuka makubaliano ya mkataba wa mnada wa korosho, ambao alitaka korosho walizonunua zisitoke nje ya mkoa huo hadi pale watakapokuwa wamelipa fedha hizo walizokuwa wakidaiwa.

“Kampuni ya Alpha imefanikiwa kulipa deni walilokuwa wakidaiwa kwa hiyo kwa sasa hatuna tatizo nao huku Kaasal wakitoa kiasi na kusema kuwa watamalizia deni lao mara moja mkoa unataka kila mtu apate haki yake bila ya kudhulumiwa hivyo makampuni mengine yasifanye mchezo kama huo,” alisema Ndikilo.

Hata hivyo, alizipongeza kampuni hizo kwa kutekeleza agizo lake ambapo fedha walizotoa tayari zimepewa walengwa ambao ni wakulima, ambao wamefurahia malipo hayo ambapo kwa mwaka huu wakulima wamepata mazao mengi na bei nzuri.

Alisema kampuni hizo zilinunua tani 1,930.9 ambapo kampuni ya kwanza ilinunua tani 1,430 zenye thamani ya Sh 4,202,514,402 huku ya pili ikinunua tani 500.037 zenye thamani ya Sh 1,591,608,288 ambapo kampuni ya kwanza ilitakiwa kulipa fedha hizo Novemba 23, mwaka huu.

Aidha, alisema kampuni ya pili ilItakiwa kulipa Novemba 16 mwaka huu, lakini hadi wiki iliyopita walikuwa hawajalipa na kuvunja taratibu za makubaliano ya mnada ambazo zinamtaka mnunuzi baada ya kushinda zabuni anatakiwa kulipa baada ya siku saba.

SOURCE HABARI LEO

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *