Makala

USICHUKULIE KAWAIDA, DALILI HIZI ZAWEZA KUWA NI MWANZO WA UPOFU.

DALILI hizi zinaweza kuchukuliwa kawaida na watu wengi, lakini kumbe laiti wangejua kuwa ni miongoni mwa visababishi vya uoni hafifu!

Nazo ni pamoja na macho kuwasha, kutoka machozi, kuogopa mwanga, jicho kuwa jekundu na mtu kufikicha macho kila wakati. Wapo watu wengine ambao hukumbwa na matatizo ya kichwa kuuma lakini mara nyingi hukimbilia kupima au kunywa dawa za malaria. Lakini pia wapo ambao hawapati dalili za wazi mpaka pale wanapofika hatua ya kuwa kipofu kabisa ndipo huenda kwa wataalamu wa macho lakini bila mafanikio ya kupona.

Hapo ndipo Mratibu wa magonjwa ya macho Mkoa wa Tabora, Dk Mathias Sosoma anatamani jamii ingetambua umuhimu wa kuangalia afya ya macho kila mara. Kwa kuchunguza afya ya macho mara kwa mara, watu wengi waliopata upofu wasingekumbwa na tatizo hilo. Wasingeathirika kiungo hicho muhimu katika maisha ya wanadamu; kwani upofu umekuwa sehemu ya vichocheo vya umasikini kwa mtu binafsi na hata kwa familia.

Hali inakuja hasa pale mtu anayetegemewa anapokosa kuona, ina maana hakuna kitakachofanyika kwani yeye hugeuka kuwa mtegemezi kwa kila jambo nje na ndani ya familia. Ushauri wa Dk Sosoma unazingatia takwimu za mkoa huo wa Tabora kupitia upimaji wa macho uliofanyika hivi karibuni. Miongoni mwa watu 13,421 waliojitokeza kupima afya ya macho tangu Januari hadi Septemba mwaka huu, 1,015 walibainika kuwa na tatizo na wakapatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyu wa macho, takwimu za kitaifa zinaonesha Watanzania asilimia 0.7 wana upofu wa macho na asilimia 2.1 wana uoni hafifu hali ambayo jamii inasisitizwa kujitokeza kupima afya ya macho.

Uoni hafifu

Anaelezea uoni hafifu kuwa ni upungufu wa uwezo wa kuona au kushindwa kuona herufi maalumu iliyopo umbali wa meta 6. Mtu mwenye uoni mzuri anaweza kuona herufi hiyo akiwa umbali wa meta 18 .

“Visababishi vya uoni hafifu ni pamoja na macho kuwasha, kutoka machozi, kuogopa mwanga, jicho kuwa jekundu na mgonjwa anakuwa na hali ya kujikuna kila wakati machoni,” anasema Dk Sosoma. Hali hiyo ya kukuna macho, husababisha kioo cha jicho kuvimba, na kufanya asione vizuri. Pia kwa sababu ya kukuna mara kwa mara, anaweza kupata vidonda na baadae kupata kovu kwenye kioo cha jicho.

Kichwa kuuma ni miongoni mwa dalili za matatizo ya uoni hafifu ingawa wapo ambao hawapati dalili hadi hapo anapokumbwa na tatizo la upofu moja kwa moja. Tiba kwa mtu mwenye matatizo hayo, ni dawa za matone ikiwemo aina ya timolol pamoja na kuambatana na upasuaji. Hata hivyo mgonjwa akifikia kwenye upofu, mtaalamu huyu anasema hata akifanyiwa matibabu hawezi kurudia hali yake ya awali ya uoni wa kawaida wa siku zote.“Kwa hiyo ni bora kufanya uchunguzi wa shinikizo la jicho walau mara mbili kwa mwaka ili uweze kugundulika mapema,” anashauri.

Mtoto wa jicho

Tatizo hili pia ni miongoni mwa yanayokabili macho. Huwapata watu wa rika zote. Tatizo linaweza kuwa la kuzaliwa au baada. Dalili zake ni uoni hafifu ambao huongezeka polepole mpaka kufika upofu kabisa. Kunakuwapo na kitu ambacho huota katikati ya mboni ya jicho.

Shinikizo la jicho

Hili pia huathiri watu wote kuanzia watoto hadi wazee. Hutokana na mkandamizo mkubwa wa jicho zaidi ya kiwango cha kawaida. Hutokana na kiwango cha maji na ute kwenye jicho yanayozalishwa na kutolewa kwenye jicho, yakawa kwenye kiwango cha kawaida lakini hayatoki bali yanabaki ndani ya jicho. Pia kutokana na kiwango kikubwa, husababisha kandamizo ndani ya jicho na kuathiri mshipa wa fahamu wa jicho.

Wenye tatizo hili wanaweza kuzaliwa nalo, kupata kwenye umri mkubwa, kutokana na ajali ya kwenye jicho, uambukizo wa jicho baada ya upasuaji wa kutoa mtoto wa jicho. Visababishi vingine ni ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, msongo wa mawazo na kutumia dawa za macho zenye vichocheo kwa muda mrefu. Dk Sosoma anasema tatizo hili hutokea kwa kuathirika kwa mishipa ya fahamu ya jicho au retina. Hali hii husababishwa na kuumia kwa njia ya mishipa ya fahamu au kuvimba kwa mshipa wa fahamu wa jicho.

Sababu nyingine za hali hii ni unyafuzi, upungufu wa vitamin B, sumu itokanayo na tumbaku na mihogo isiyoandaliwa vizuri pamoja na dawa kama vile kwinini. Aidha visababishi vingine ni maambukizi hasa ya surua, uti wa mgongo, kaswende, homa ya matumbo, magonjwa ya mfumo wa damu, kisukari na shinikizo la damu lililozidi kiwango. Vingine ni majeraha ya kichwa, uvimbe kwenye njia ya mshipa ya fahamu ya jicho na shinikizo la jicho.

Uoni hafifu unaohitaji mtu avae miwani katika shughuli zake za kila siku umegawanyika katika makundi matatu. Nayo ni, wenye uwezo wa kuona mbali, kuona karibu ambalo huathiri watu wa rika zote yaani watoto na wakubwa.

Kundi la wenye kuhitaji miwani wakati wa kusoma ni kwa wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea. Katika kuelezea hali ya magonjwa ya macho mkoani Tabora, mtaalamu huyu anasema ambayo wamebaini kutokana na wagonjwa wanaofika kupima, yametokana na mzio, mtoto wa jicho, matatizo yanayohitaji uvaaji miwani na shinikizo la jicho (Glaucoma). Wengine ni kutokana na ajali mbalimbali za macho, matatizo kwenye mishipa ya fahamu na pazia lake (retina), kovu kwenye kioo cha jicho na makengeza.

Aidha watu wenye ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, wamekuwa wakisisitizwa kujitokeza kupima macho angalau mara moja kwa mwaka. Kikubwa anachoshauri jamii ni kuepuka kununua miwani kabla ya kuonana na wataalamu waliosomea ili waweze kuwashauri na kuwapima na kujiridhisha tatizo walilo nalo. Vile vile anasisitiza kuwa, siri ya matibabu ya macho ni kuwahi kwa wataalamu wa macho mapema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi unaotakiwa na kupata tiba haraka.

Pia anashauri mwenye tatizo la macho kabla ya kununua dawa, aende kwanza aonane na wataalamu wa macho au kliniki za macho zinazotambulika. Kwa upande wa mkoa wa Tabora, kliniki zipo hospitali ya rufaa Mkoa wa Tabora Kitete na hospitali ya rufaa ya misheni ya Nkinga. Wenye ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, wanashauriwa kuonana na madaktari wa macho na kufanyiwa kipimo maalumu mara moja au mara mbili kwa mwaka kubaini athari za magonjwa kabla hayajaathiri jicho katika kiwango cha juu.

Pamoja na hamasa kwa jamii kujitokeza kupima macho, Dk Sosoma anasema mkoani humo wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa wataalamu. Wilaya nyingi hazina wataalamu waliobobea kwenye afya ya macho. Pia upo upungufu wa dawa za macho na ukosefu wa vifaa tiba muhimu. Kingine ni ukosefu wa huduma za mkoba (kuwafikia wenye matatizo walipo).

Hivyo wagonjwa wasio na uwezo wa kufuata huduma, hubaki na upofu unaotibika pasipo kupata huduma kwani kama kungekuwa na huduma za mkoba wagonjwa wengi wangefikiwa na kupata huduma hiyo na kupona. Changamoto nyingine ni ukosefu wa wafadhili katika huduma za afya ya macho hususani kwa wazee wasiojiweza. Lakini pia anasema, uelewa wa jamii katika matatizo ya macho na jinsi ya kutibu uko chini.

Sehemu kubwa ya watu, wanatajwa kuwa huwa wanakwenda kujinunulia dawa za macho bila ushauri wa wataalamu. Kwa ujumla, mtaalamu huyu wa macho anahimiza jamii kujengwa uelewa juu ya afya ya macho kupitia njia mbalimbali ikiwamo vyombo vya habari. Kwa kufanya hivyo, anaamini itafumbua wengi kufahamu dalili na athari za kuchelewa kutibiwa.

SOURCE HABARI LEO

Show More

komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close