Ujasiriamali

Zao la muhogo linavyoweza kupaisha uchumi wa wakulima

TANZANIA ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa muhogo hata kuongoza katika Afrika kutokana na kuwa na utajiri wa ardhi kubwa yenye rutuba.

Takwimu kutoka Wizara ya Kilimo zinaonesha mwaka 2005 Tanzania ilizalisha tani milioni 1.8 za muhogo mkavu, mwaka 2006 katika nchi nzima zilivunwa tani milioni mbili za muhogo mkavu. Hivyo, ili kuingia katika biashara ya muhogo ambao una soko kubwa duniani inabidi kuzalisha zao hilo kwa wingi.

Hata hivyo, unga wa muhogo wenye ubora wa hali ya juu na unaokubalika katika soko la kimataifa ni ule ambao haujavundikwa na unaweza kutumika katika kutengeneza vitu mbalimbali kama vile ugali, biskuti, mikate, keki, maandazi, chapati na vyakula vingine. Wataalamu wa kilimo wanasisitiza kuwa tangu kuvuna muhogo shambani kwa njia ya kisasa hadi kutengenezwa unga, inatakiwa muda uwe mfupi usiozidi saa 24.

Kulingana na teknolojia ya hivi sasa, muhogo ukishavunwa husafishwa na kuingizwa katika mashine maalumu ili kukatwa katika vipande vidogo na hatua inayofuatia ni kwenda kukamua ili kupunguza maji kwa asilimia 80 na kuanika kwenye jua baada ya saa moja tu unga safi unakuwa umekauka. Muhogo uliosindikwa ili uweze kuuzwa nje ya nchi ni lazima uwe mweupe, usiwe na mabonge, uwe na ladha nzuri, usiwe na uvundo kwa maana kwamba, unyevu upunguzwe hadi kufikia asilimia 11 na uwe umethibitishwa na Shirika la Viwango nchini(TBS).

Zao hili lina uwezo wa kuwakomboa wananchi kiuchumi kutokana na utafiti kuonesha kuwa bidhaa zaidi ya 300 zinaweza kuzalishwa kutokana na muhogo. Mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa muhogo. Hata hivyo, wameshindwa kufanya kilimo cha muhogo kuwa cha kibiashara kutokana na kukosa maelekezo ya kitaalamu na hivyo kufanya zao hilo libaki kuwa la chakula.

Nathaniel Lugongo ni kiongozi wa asasi ya Mwangaza Foundation katika Wilaya ya Nyasa ambaye anasema muhogo ndiyo zao kuu la chakula mwambao mwa ziwa Nyasa, wamedhamiria kulifanya zao hili kuwa la kibiashara. Kwa mujibu wa Lugongo kinachohitajika hivi sasa ni kupata mashine ya kusaga mihogo mibichi kuwa unga badala ya mtindo uliozoeleka wa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa ambao wanailoweka mihogo baada ya kumenya maganda kwenye vyungu kisha kuianika juani kabla ya kuisaga kwa mashine au kutwangwa kwenye kitu.

“Soko la unga wa muhogo ndilo tatizo kubwa hivyo endapo mihogo mibichi itaanza kusagwa kwa mashine za kisasa itaweza kuwa na soko kubwa na kuinua hali ya uchumi kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa’’, anasisitiza Lugongo. Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani ilikaririwa ikitangaza kuwa nchini Msumbiji kuna kiwanda cha kutengenezea pombe aina bia ya kisasa kutokana na muhogo.

Pombe hiyo inauzwa ndani na nje ya nchi ya Msumbiji, hali ambayo imesababisha muhogo katika nchi hiyo kuwa zao la kibiashara kwa kuwa wakulima wanapata faida kubwa kutokana na kuuza unga wa muhogo unaozalishwa kutokana na mihogo mibichi katika viwanda nchini humo.

Serikali kwa kutumia vikao vya ujirani mwema inaweza kwenda kujifunza nchini Msumbiji pamoja na wataalamu wa kilimo kwa kutembelea kiwanda cha bia zinazotokana na mihogo ili utaalamu huo ufike nchini hatimaye, wakazi wa Nyasa na watanzania kwa ujumla waweze kufanya muhogo kuwa ni kilimo cha kibiashara. Inakadiriwa ili kujenga kiwanda kidogo cha kisasa cha kusaga mihogo mibichi kwa ajili ya kupata unga, zinahitajika jumla ya Sh milioni 100 na kwamba wakulima kazi yao itakuwa ni kumenya mihogo na kupeleka kiwandani.

Utafiti unaonesha kuwa soko la unga wa mihogo mibichi inayomenywa na kutengeneza unga kiwandani ni kubwa nje ya nchi ikiwemo Afrika Kusini na nchi za Afrika Magharibi. Ukitembelea mwambao mwa ziwa Nyasa kuna baadhi ya wakulima wamelima mihogo kati ya miaka mitatu hadi mitano iliyopita hadi sasa ipo shambani haijavunwa kutokana na kukosa soko la uhakika la unga ambao unazalishwa kwa kusindika badala ya kupelekwa moja kwa moja kiwandani.

Mkoa wa Mtwara unakadiriwa kuzalisha asilimia 28 ya muhogo nchini, lakini bado kiwango hicho kinachozalishwa hakimnufaishi mkulima wa Mtwara kutokana na changamoto nyingi zinazoukabili mfumo mzima wa uzalishaji na usindikaji wa zao hilo. Mikoa inayozalisha muhogo kwa wingi ni Mwanza, Mtwara, Lindi, Shinyanga, Tanga, Ruvuma, Mara, Kigoma, Pwani na karibu maeneo yote ya Zanzibar.

Kanda ya Ziwa ni wazalishaji wakubwa zaidi ikifuatiwa na ukanda wa Kusini, ambako Mkoa wa Ruvuma huzalisha asilimia 10 ya uzalishaji wote nchini. Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), muhogo ni zao la tatu kwa kuwa na kiwango kikubwa cha wanga katika nchi za ukanda wa joto, zikiwemo nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara. Takribani watu milioni 500 duniani hutegemea zao hilo kama chakula kikuu.

Kulingana na FAO, uzalishaji wa muhogo duniani ulikadiriwa kuwa tani milioni 184 mwaka 2002, kiwango ambacho baadaye kiliongezeka hadi kufikia tani milioni 230 mwaka 2008. Katika Afrika, mwaka 2002 jumla ya tani milioni 99.1 zilizalishwa na Bara la Asia lilizalisha tani milioni 51.5 na tani milioni 33.2 zilizalishwa huko Latin America na Caribbean. Takwimu za FAO zinaonesha kuwa Thailand ndiyo inayoongoza kwa kuuza nje zao la muhogo uliokaushwa.

Asilimia 77 ya muhogo uliouzwa nje kwa mwaka 2005 ulitoka nchini humo. Nchi ya Vietnam imewahi kuweka rekodi ya kuuza zao la muhogo kwa asilimia 13.6 ya mahitaji duniani, ikifuatiwa na Indonesia asilimia 5.8 na Costa Rica asilimia 2.1. Takwimu za mwaka 2005 zinaonesha kuwa Tanzania ilizalisha muhogo kwa wastani wa tani milioni mbili tu kwa mwaka kwa hekta ambapo wastani wa Bara la Afrika mwaka huo ulizalisha muhogo tani milioni 3.3 kwa mwaka na nchi ya Nigeria ilizalisha tani milioni 4.7 kwa mwaka.

Nchini Nigeria, serikali imetunga sheria kwa kila anayetengeneza mikate, biskuti na bidhaa nyingine achanganye na unga wa muhogo kama njia ya kulinda soko la unga wa muhogo na kuwapa wakulima hamasa ya kuendelea kulima zao hilo katika nchi hiyo. Nchi za Afrika ambazo zina viwanda vikubwa vya kusindika zao hili ni Afrika Kusini, Nigeria na Ghana. Hapa nchini, zao hili linaweza kutumika kutengenezea pombe, kwenye viwanda vya bia na dawa nyingine viwandani.

Kasam Maswaga ambaye ni mtaalamu wa kilimo anasema elimu ya kusindika muhogo ikienea katika maeneo mengi nchini miaka 10 ijayo zao la muhogo litakuwa ni kubwa na lenye heshima katika kuinua kipato cha mkulima kwa kulifanya kuwa la chakula na biashara. “Sisi wataalamu wa kilimo na serikali kwa ujumla tumelenga kuhakikisha zao la muhogo kupitia usindikaji linatumika kama zao la chakula na biashara kwa sababu hivi sasa tunaendelea kutoa mafunzo ya namna ya kulisindika na kulitumia,” anasema Maswaga.

Utafiti umebaini kuwa zao hili ni chakula kikuu kwa kuwa karibu watu bilioni moja katika nchi zaidi ya 105 duniani wanatumia. Muhogo huchangia theluthi moja ya mahitaji ya virutubisho vya kuongeza nguvu mwilini. Zao la Muhogo kwa mara ya kwanza lililetwa na Wareno katika Afrika. Zao hili hulimwa nchi zaidi ya 34 za Afrika kwenye eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari milioni 200. Tanzania inatajwa kuwa nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani. Karibu hekta 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo.

Zao hili linachangia karibu asilimia 15 ya chakula kwa nchi nzima. Inakadiriwa kuwa takribani kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini . Hapa nchini muhogo unatajwa kuwa zao la pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 19 baada ya mahindi. Wanga wa muhogo hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali katika kuta za nyumba na sukari. Muhogo una kiasi kikubwa cha vitamini A na kiasi kidogo cha protini.

Ulaji wa mihogo husaidia walaji kuepukana na ugonjwa wa ukavu macho. Pia majani ya mihogo huweza kutumika kama mboga za majani yaani kisamvu. Mpaka sasa wataalamu wanataja aina mbili za mbegu bora za muhogo ambazo zimethibitishwa baada ya kufanyiwa utafiti na kubaini kuwa mbegu hizo huvumilia magonjwa na kuzaa sana ukilinganisha na mbegu za kienyeji. Mbegu hizo ni aina ya Naliendele na mbegu aina ya Kiroba ambazo huzaa kati ya tani 25 hadi 30 za muhogo kwa hekta moja, pia zinaweza kuvunwa kuanzia miezi 9 toka kupandwa.

SOURCE HABARI LEO.

Show More

komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close