Home / Habari Za Kitaifa / MVUA YAACHA VILIO, 250 WAKOSA MAKAZI SUMBAWANGA.

MVUA YAACHA VILIO, 250 WAKOSA MAKAZI SUMBAWANGA.

WATU 250 wamekosa makazi ya kudumu baada ya nyumba zao zipatazo 43 kuharibiwa, huku mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka sita akijeruhiwa kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali kunyesha.

Mvua hiyo ilinyesha katika vijiji vya Mpwapwa na Jangwani vilivyopo katika Kata ya Mpwapwa katika Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpwapwa, Marekani Kayembe alisema mvua hiyo iliyodumu kwa zaidi ya saa tatu ilianza saa nane usiku wa kuamkia Desemba 23 ilisababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa vijiji hivyo ambapo baadhi ya kinamama na watoto walilazimika kujificha uvunguni mwa vitanda.

Alisema mvua hiyo iliezua paa na kuangusha kuta za nyumba 24 kijijini hapo huku ikiwaacha watu wapatao 120 wakiwa hawana makazi ya kudumu ambapo wengi wao wamejihifadhi kwa majirani na ndugu zao wa karibu ambao nyumba zao hazikuharibiwa na mvua hiyo.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mpwapwa, Upendo Winga alikiri kumpokea mtoto Edson Konstebo (6) saa 11 alfajiri akiwa amepoteza fahamu.

Alisema mtoto huyo alikuwa amejeruhiwa kichwani baada ya kuangukiwa na tofali kufuatia kubomoka kwa ukuta wa nyumba alimokuwa amelala.

Naye Bahati Mangula alisema mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali ilisababisha taharuki kwa wakazi ambapo yeye na watoto wake wawili walisalimika, kwani walijificha uvunguni mwa kitanda wakati ukuta wa nyumba yao ulipoanguka.

Waathirika waliozungumza na gazeti hili walidai kuwa mvua hiyo imewasababishia hasara kubwa kwani licha ya kubomoa nyumba zao pia imeharibu vyakula na mali nyingine.

Diwani wa Kata ya Mpwapwa, Abel Kambaulaya amewaomba wasamaria wema kutoa msaada wa hali na mali kwa waathirika hao ambao nyumba zao na vyakula vyao vimeharibiwa na mvua hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani Haule akiwa ameongozana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya alisema wiki iliyopita mvua iliyoambatana na upepo mkali iliharibu nyumba 27 katika kijiji cha Mwela kilichopo katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga.

Alisema Serikali wilaya imetoa msaada wa gunia moja la mahindi kwa mtoto aliyejeruhiwa baada ya kuangukiwa na tofali katika Kijiji cha Mpwapwa ambaye anaishi na bibi yake.

SOURCE HABARI LEO.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Historia ya marehemu Isaac Nyagabona Muyenjwa Gamba

HISTORIA YA MAREHEMU ISAAC NYAGABONA MUYENJWA GAMBA. Ratiba Kwa Ufupi Jumatatu Alfajiri – Kupokea Mwili Airport …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *