Home / Habari za Kimataifa / UDUKUZI WA URUSI: BIDEN AMTAKA TRUMP ‘AKOMAE’

UDUKUZI WA URUSI: BIDEN AMTAKA TRUMP ‘AKOMAE’

Bw Biden amesema wakati umefika Trump “kuwa mtu mzima”

Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden amemwambia Rais mteule wa Marekani Donald Trump kwamba anafaa “kukomaa” na akamshutumu kwa kukosoa majasusi wa Marekani.

Leo Ijumaa, Bw Trump anatarajiwa kupashwa habari za kijasusi kuhusu tuhuma kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa urais wa Marekani uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana.

Lakini Bw Trump ametilia shaka madai kwamba Urusi ilihusika, na badala yake akawakosoa vikali majasusi wa Marekani kwenye Twitter.

Bw Biden amesema ni jambo la kusikitisha kwa rais mteule kutokuwa na imani na mashirika ya kijasusi.

“Kwa rais kutokuwa na imani na, na kutokuwa tayari kuyasikiliza, mashirika ya ujasusi, kuanzia majasusi wa jeshi hadi majasusi wa CIA, ni jambo la kukosa hekima kabisa,” alisema kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha PSB.

“Wazo kwamba unaweza kuwa na ujuzi au ufahamu zaidi ya mashirika ya kijasusi – ni kama kusema kwamba ninafahamu fizikia zaidi ya profesa wangu. Sikusoma kitabu, ninajua tu kwamba ninajua zaidi.”

Alipoulizwa anafikiria nini kuhusu hatua ya Bw Trump kushambulia mashirika ya kijasusi na makundi mengine kwenye Twitter mara kwa mara, Bw Biden alisema: “Komaa Donald, komaa, ni wakati wa kukomaa na kuwa mtu mzima, wewe ni rais. NI wakati wa kufanya jambo la busara. Tuonyeshe sifa zako.”

Baadaye, alimweleza Bw Trump kama “mtu mzuri”.

Lengo la udukuzi lilikuwa nini?

Bw Biden amesema ameshasoma ripoti ya mashirika ya ujasusi ya Marekani ambayo inaonyesha wazi kuhusika kwa Urusi katika udukuzi kadiri uchaguzi ulivyokaribia.

Bw Trump atapashwa habari kuhusu ripoti hiyo leo Ijumaa.

Baadaye, nakala ya ripoti hiyo – ambayo imetolewa baadhi ya maelezo – itafanywa wazi kwa umma wiki ijayo.

Bw Biden amesema ripoti hiyo inaeleza wazi “walichofanya Warusi, kama sehemu ya sera yao, kujaribu kuathiri na … kutia doa shughuli za uchaguzi Marekani”.

Amesema udukuzi wa barua pepe ulikuwa sehemu ya kampeni ya kutatiza juhudi za kampeni za Hillary Clinton, mpinzani wa Bw Trump kwenye uchaguzi wa urais.

Ameongeza kwamba udukuzi huo ulikuwa umeenea sana kinyume na ilivyodhaniwa awali.

Miongoni mwa watu ambao barua pepe zao zilidukuliwa ni John Podesta, meneja wa kampeni wa Bi Clinton.

Sava za Kamati Kuu ya Taifa ya chama cha Democratic pia ilidukuliwa.

Nyaraka hizo baadaye zilifichuliwa kwenye mtandao wa Wikileaks.

Alhamisi, mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa Jenerali James Clapper, aliambia kikao cha Kamati ya Huduma za Jeshi katika Seneti kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin aliagiza kufanyika kwa udukuzi huo.

Alisema lengo lake na azma katika udukuzi huo vitafichuliwa wiki ijayo.

Urusi imekanusha tuhuma hizo kwamba ilihusika katika udukuzi huo. Hata hivyo, Marekani tayari imetangaza kuwawekea vikwazo baadhi ya maafisa wakuu wa Urusi.

Bw Trump mara kwa mara amekanusha madai kwamba serikali ya Urusi ilidukua tarakilishi za Bw Podesta na sava ya Kamati Kuu ya Taifa ya chama cha Democratic.

Jumatano, alirejelea pendekezo lake kwamba huenda “mtoto wa miaka 14” alitekeleza udukuzi huo.

Alhamisi, alisema yeye ni “shabiki mkuu” wa mashirika ya ujasusi, baada yake kutilia shaka kwa muda mrefu tuhuma za kuhusika kwa Urusi.

Hata hivyo, baadaye aliibua maswali kuhusu jinsi chama cha Democratic kilishughulikia udukuzi huo.

“Ni jinsi gani na ni kwa nini wana uhakika hivyo kuhusu udukuzi ikiwa hawakuitisha uchunguzi ufanywe kwenye sava zao za kompyuta? Nini kinaendelea hapa?” aliuliza kwenye Twitter.

Mr Trump alikuwa ameahidi kutoka “maelezo mabya” kuhusu madai hayo ya udukuzi wiki iliyopita.

Lakini hilo halikufanyika.

Bw Trump ataapishwa kuwa rais tarehe 20 Januari.

 SOURCE BBC SWAHILI.

About komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Check Also

Mohamed Bin Salman

CIA ‘yamlaumu mwanamfalme wa Saudia ‘

Shirika la ujasusi la Marekani(CIA) linaamini kuwa Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa Saudi Arabia ndiye …

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *