Makala

MCHANGO WA MWANAMKE KWENYE KILIMO UTAMBULIWE.

MCHANGO wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo nchini umeendelea kuongezeka katika miaka ya hivi karibuni ambapo katika kipindi cha mwaka 2015, kilimo kilichangia asilimia 29 ya pato ghafi la taifa ikilinganishwa na asilimia 28.8 kwa kipindi cha mwaka 2014.

Hiki ni kiwango cha juu kabisa cha uchangiaji ikilinganishwa na sekta nyingine kwa mujibu wa ripoti ya Uchumi Tanzania 2016. (Report on Tanzania Economic Outlook 2016, Delloite: June 2016). Hivyo sekta ya kilimo ina mchango mkubwa katika kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la umaskini katika jamii ya Watanzania.

Tanzania inatambua kuwa usawa wa kijinsia unawezesha wanaume na wanawake kushiriki kikamilifu katika michakato ya kimaendeleo. Mbali na kutambua huko, sekta ya kilimo hapa nchini bado ni baguzi ambapo wanawake hawapati fursa zilizopo na mgawanyo wa rasilimali kwa usawa.

Mkinzano uko wazi ukizingatia kuwa zaidi ya asilimia 90 ya nguvu kazi katika kilimo ni mwanamke ambaye huzalisha takribani asilimia 70 ya mahitaji ya chakula nchini (Kitabu ya Mmasa JJ ya Ushiriki wa mwanamke katika Kilimo Tanzania-2013).

Hivi karibuni, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano (SJMC) iliyopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakishirikiana na Shirika la Land O’Lakes waliandaa semina kwa waandishi wa habari kuhusu Usawa wa Kijinsia katika Kilimo, Usalama wa Chakula na Lishe iliyofanyika Iringa.

Waandishi hao waliweza kujifunza ni kwa namna gani sera na sheria zinamsaidia na kumkandamiza mwanamke na mwanamume katika mnyororo wa thamani wa shughuli za kilimo.

Vile vile imani na mila potofu ambazo zinamkandamiza mwanamke na kumfanya ashindwe kushiriki kikamilifu kwenye kilimo pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa wanawake katika sekta hiyo.

Mgawanyo wa majukumu baina ya wanawake na wanaume katika shughuli za kilimo, nani anawekeza nguvu kubwa na nani anafaidika zaidi, ikiwa ni pamoja na mchango wa wanawake katika usalama wa chakula na lishe katika kaya.

Hivyo ukweli wa mwanamke kutumia muda mwingi katika uzalishaji wa mashambani unathibitishwa na mkulima Neema Ngengena ambaye ni kibarua katika shamba la Jesca Msambatavangu, lililopo Kijiji cha Mgela, Iringa Vijijini, Iringa, anayesema kuwa maisha magumu yamemfanya afanye kibarua kinachompatia ujira wa Sh 3,000 kwa siku, fedha anazozitumia kujikimu na familia yake.

Anasema wakati akiwa anafanya kibarua katika shamba hilo, mumewe hushughulikia shamba la familia ambapo naye huungana naye pale anapopata muda, lengo ni kuongeza kipato cha familia.

Msambatavangu anasema anatoa ajira kwa wanakijiji wanaokwenda kumsaidia katika shamba lake kwa lengo la kutafuta fedha za kuwezesha kumudu maisha yao.

Pia mwanamke huyo pia ana shamba darasa ambapo wastani wa wanakijiji 400 hufika kwa ajili ya kujifunza.

Shamba hilo linafadhiliwa na taasisi ya Bill Clinton. Msambatavangu mwenye shamba la eka 60 ambazo hutumia kulima mahindi, alizeti, soya na maharage ambapo ekari moja humpatia gunia 27 mpaka 30.

Anasema mafanikio yake yametokana na wazazi wake waliomuwezesha kujua mbinu mbalimbali za kupiga hatua za maendeleo, kwani pamoja na kuwa na shahada ya uzamili lakini bado yupo shambani.

Anapoelezea safari ya mafanikio katika kilimo, anasema katika ghala lake ana gunia 600 za mahindi na 450 alizozivuna kwenye shamba lake, na kuwa kiasi kikubwa cha mazao anayoyapanda anatumia kulisha wanafunzi katika shule yake anayomiliki na sehemu inayobaki anaweza kuuza na kujipatia kipato.

Anapozungumzia changamoto, Msambatavangu anasema ucheleweshwaji wa pambejeo za kilimo ni tatizo ambalo linawasumbua wakulima wengi akiwamo na yeye na kutaka wizara husika kuwa na ufuatiliaji wa karibu.

Ni mwaka wa sita kwa mkulima huyo katika kilimo na ndoto yake ni kufika mbali zaidi kwa kulima kilimo cha kisasa kinachotumia teknolojia ya kisasa huku akiwatia moyo wanawake kuwa wanaweza kufanikiwa hata kama mila na desturi zimekuwa zikiwakandamiza.

“Mama siku zote ataficha chakula kwa ajili ya familia. Wanaume wanawaza kuuza na kuoa,” anasema.

Anapozungumzia suala la mikopo, anasema taasisi nyingi za fedha, ikiwa ni pamoja na benki ya kilimo zimekuwa mjini wakati wakulima wengi wako vijijini na kushauri kuwa na matawi kwenye mikoa ya kilimo.

“Tutoe kipaumbele kwenye mikoa inayohusika na kilimo,” anasisitiza lakini anatoa angalizo kuwa wakulima wengi wadogo hawawezi kukopa kutokana na masharti yaliyopo.

Mratibu Ubunifu wa Kijinsia katika kuleta uhakika wa usalama wa chakula wa Shirika la Land O’Lakes, linalofanya shughuli zake katika mikoa ya Iringa, Morogoro na Mbeya, Mary Kabelele anasema wapo kwa ajili ya kuangalia ni jinsi gani wanaweza kumsaidia mwanamke katika kilimo.

Anasema wameweza kuangalia sera, sheria na kanuni zinazoweza zinasaidia ama kukandamiza mwanamke katika sekta ya kilimo.

Mshauri huru wa kitaalamu katika utawala bora, jinsia na maendeleo, Magreth Henjewele anasema wanawake ambao asilimia kubwa inatumia nguvu kazi yao katika kilimo wanaweza kuboresha lishe katika kaya.

“Huzalisha karibu chakula chote, hivyo wana nafasi muhimu nchini ikizingatiwa kwamba asilimia 35 ya watoto chini ya miaka mitano wana tatizo la udumavu na asilimia 16 wana tatizo ukondefu.

Anasema vitamini na madini zinahitajika katika afya na ukuaji wa ubongo na kwamba ubongo wa mtoto hukua haraka wakati wa ujauzito na miaka miwili baada ya kuzaliwa.

“Lishe duni wakati wa ujauzito na miaka miwili ya mwanzo baada ya mtoto kuzaliwa husababisha madhara ya kiafya yasiyorekebishika na kupunguza uwezo wa mtoto kujifunza shuleni,” anasema.

SOURCE HABARI LEO.

Show More

komaji

Naitwa Ramadhani Shabani Komaji , Ni kijana wa Kitanzania mwenye upendondo na Kila Mwanadamu , Amani upendo furaha ndiyo Faraja ya maisha yangu, Tovuti yetu inazungumzia mambo yote ya kijamii na Kiimani mwenye kupenda kuchangia maendeleo na uboreshaji wa Tovuti yetu twamkaribisha sana +255655004100

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close